Kanisa la Anglikana lamtunuku Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba cheo cha Lay Canon

■Ni mara ya kwanza kutolewa kwa kiongozi asiyekuwa Muumini wa Kanisa hilo

DODOMA-Kanisa la Anglikana Tanzania limemtunuku Waziri Mkuu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, cheo cha Lay Canon kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuhamasisha na kufanikisha uchangishaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na vitega uchumi vya kanisa hilo.
Dkt. Nchemba ametunukiwa heshima hiyo leo katika hafla ya uchangishaji fedha iliyofanyika katika Kanisa Anglikana, Jimbo la Dodoma. Tuzo hiyo ni ishara ya kuthamini juhudi zake za kuunga mkono maendeleo ya taasisi za dini na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dkt. Maimbo Mndolwa, alisema kuwa mchango wa Waziri Mkuu umeonesha mfano wa uongozi unaojali maendeleo ya jamii na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini.

Alieleza kuwa juhudi za Dkt. Mwigulu zimekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha upatikanaji wa rasilimali za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuimarisha uwezo wa kanisa kujitegemea kiuchumi na kuboresha huduma za kijamii.

Dkt. Mndolwa aliongeza kuwa uwekezaji unaofanywa na kanisa kupitia miradi yake ya kiuchumi utasaidia kuongeza mapato, kuimarisha huduma za elimu, afya na maendeleo ya jamii, pamoja na kuchochea ustawi wa waumini na wananchi kwa ujumla.

Cheo cha Lay Canon ni miongoni mwa vyeo vya juu vinavyotolewa na Kanisa la Anglikana kwa waumini waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kanisa na jamii. 

Kutunukiwa kwa Dkt. Mwigulu licha ya kutokuwa muumini wa kanisa hilo kunadhihirisha kutambuliwa kwa mchango wake katika kuimarisha shughuli za maendeleo ya kanisa na mshikamano kati ya viongozi wa dini na Serikali kwa manufaa ya Watanzania wote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here