Kombe la Dunia 2026:Ghana yaibuka na ushindi wa dakika za mwisho bao 1-0 dhidi ya Panama

NA DIRAMAKINI

TIMU ya taifa ya Ghana imeanza kampeni yake ya Kombe la Dunia 2026 kwa ushindi muhimu wa bao 1-0 dhidi ya Panama.
Ni baada ya Caleb Yirenkyi kufunga bao la ushindi katika dakika za nyongeza za kipindi cha pili kwenye mchezo wa Kundi L uliochezwa jijini Toronto,Canada.

Bao hilo la dakika za mwisho lilisababisha shamrashamra kubwa miongoni mwa mashabiki na wachezaji wa Ghana, huku likihitimisha mchezo uliokuwa na ushindani mkali na kuipa timu hiyo pointi tatu muhimu katika hatua ya makundi.

Yirenkyi aliifungia Ghana bao hilo katika dakika ya tano ya muda wa nyongeza baada ya kumalizia kwa ustadi shambulizi la kushtukiza lililoanzia katika eneo la Ghana.

Katika mchakato wa bao hilo, Brandon Thomas aliokota mpira kwa kasi kupitia upande wa kushoto kabla ya kutoa pasi ya mwisho iliyomkuta Yirenkyi ambaye aliuelekeza wavuni kwa mguso wa karibu.

Mara baada ya bao hilo kufungwa, hali ya taharuki ilitokea uwanjani huku wachezaji wa pande zote wakijikuta katika msuguano mfupi kabla ya mwamuzi kupuliza filimbi ya mwisho iliyothibitisha ushindi wa Ghana.

Mchezo huo ulikuwa na sura mbili tofauti. Kipindi cha kwanza kilikuwa na kasi ndogo na nafasi chache za kufunga, huku Panama ikionekana kutawala zaidi mchezo na kuonesha nia ya kutafuta ushindi.

Dakika ya pili ya mchezo ilimshuhudia kipa wa Ghana, Lawrence Ati Zigi akiokoa hatari ya mapema baada ya kudaka kwa ustadi shuti la nguvu la Cecilio Waterman.

Panama iliendelea kutengeneza mashambulizi na katika dakika ya 38 ilipata nafasi nyingine, lakini Jiovany Ramos alikosa mwelekeo baada ya kupiga shuti lililopita pembeni mwa lango.

Licha ya ubora wa Panama katika kipindi cha kwanza, Ghana ilijikuta ikishindwa hata kupiga shuti moja kuelekea langoni, jambo lililoifanya kuwa timu ya kwanza katika Kombe la Dunia la mwaka huu kumaliza dakika 45 za kwanza bila jaribio lolote la kufunga.

Mambo yalibadilika kipindi cha pili baada ya Ghana kurejea kwa nguvu zaidi na kuanza kutawala mchezo. Nafasi ya kwanza ya maana ilikuja dakika ya 48 kupitia kichwa cha Jonas Adjetey, lakini kipa wa Panama Orlando Mosquera aliokoa kwa ustadi.

Ghana pia ilipata pigo baada ya kipa wake Lawrence Ati Zigi kushindwa kuendelea na mchezo kutokana na majeraha aliyoyapata kipindi cha kwanza.

Benjamin Asare aliingia kuchukua nafasi yake langoni na kufanya kazi nzuri ya kulinda ushindi huo muhimu.

Katika mchezo huo, Ghana ilimkosa kiungo wake tegemezi Thomas Partey ambaye hakuweza kusafiri kwenda Canada kutokana na kukosa kibali cha kuingia nchini humo kufuatia mashtaka yanayomkabili nchini Uingereza.

Hata hivyo, Partey amekanusha tuhuma hizo na anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Ghana katika michezo miwili iliyosalia ya hatua ya makundi itakayochezwa nchini Marekani.

Ushindi huo umeipa Ghana mwanzo mzuri katika kundi linalojumuisha pia England na Croatia, timu ambazo zinatajwa kuwa miongoni mwa vigogo wa kundi hilo.

Kwa mujibu wa viwango vya FIFA kabla ya kuanza kwa mashindano, England ilikuwa katika nafasi ya nne duniani, Croatia ya 11, Panama ya 34 huku Ghana ikishika nafasi ya 73.

Ghana inashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya tano katika matoleo sita yaliyopita ya mashindano hayo, huku mafanikio yake makubwa yakibaki kufika robo fainali mwaka 2010.

Panama, kwa upande wake, inacheza Kombe la Dunia kwa mara ya pili pekee baada ya kupoteza michezo yote ya hatua ya makundi katika ushiriki wake wa kwanza mwaka 2018.

Aidha,baada ya ushindi huo, Ghana sasa itaelekeza nguvu zake katika mchezo mgumu dhidi ya England utakaochezwa Foxborough, Massachusetts, Jumanne ijayo.

Nayo Panama itakuwa na kazi ya kusaka pointi zake za kwanza itakapokutana na Croatia katika mchezo mwingine wa Kundi L utakaochezwa jijini Toronto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here