NA DIRAMAKINI
JAMHURI ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Namibia zimekubaliana kuendeleza uhusiano wao wa kihistoria uliotokana na harakati za ukombozi kwa kuupa mwelekeo mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kupitia biashara na uwekezaji katika sekta kuza kimkakati.

Makubaliano hayo yamefikiwa leo Juni 20,2026Ikulu Dar es Salaam, wakati wa ziara ya kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mheshimiwa Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, kwa mwaliko wa mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Wakizungumza na waandishi wa habari, viongozi hao wamesema Tanzania na Namibia zina wajibu wa kuendeleza urithi wa ukombozi kwa kuutafsiri kuwa fursa za kiuchumi,ajira na ustawi wa wananchi wa pande zote mbili.
"Tumekuwa tukizungumza sana kuhusu uhusiano wa kihistoria, sasa ni wakati wa uhusiano huo kuleta faida za kiuchumi kwetu sote,” amesema Rais Dkt. Samia.
Amesema licha ya uhusiano imara wa kisiasa na kihistoria, kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia bado hakiakisi uwezo na fursa zilizopo baina ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Rais Nandi-Ndaitwah amesema Tanzania ina nafasi ya kipekee katika historia ya Namibia kutokana na mchango wake katika harakati za ukombozi na malezi ya viongozi wengi wa kizazi cha ukombozi wa nchi hiyo, huku akiipongeza kwa ukuaji imara wa uchumi na nafasi yake kama mshirika muhimu wa maendeleo katika ukanda.
Amesema,chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, Tanzania imeendelea kuwa mfano wa utulivu, demokrasia na ushirikiano wa kikanda ndani ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wamekubaliana kukuza ushirikiano katika biashara, uwekezaji, uchumi wa buluu, mafuta na gesi, kilimo, mifugo, uvuvi, madini, afya, elimu, utalii, usafiri wa anga, vijana, utamaduni na Kiswahili, huku Tanzania ikieleza utayari wa kujifunza kutoka Namibia katika uvuvi na uchumi wa buluu.
Marais hao pia wamekubaliana kuharakisha utekelezaji wa makubaliano yaliyopo,ikiwemo safari za ndege kati ya nchi hizo mbili, na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kikanda na kimataifa.
Marais wote wawili wameshuhudia utiaji saini wa hati nne za makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya biashara, maendeleo ya biashara ndogo na za kati; ulinzi, pamoja na ushirikiano wa miji kati ya Zanzibar na Manispaa ya Swakopmund ya nchini Namibia.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia na Rais Nandi-Ndaitwah wameshiriki Jukwaa la Biashara na Uwekezaji la Tanzania na Namibia katika Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam, lililowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi zote mbili.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Rais Dkt. Samia amesema Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, na kuikaribisha sekta binafsi ya Namibia kutumia nafasi ya Tanzania kama lango la masoko ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini, akitaja fursa zilizopo katika bandari na usafirishaji, kilimo na uongezaji thamani, mifugo, uvuvi, mafuta na gesi, madini, viwanda na huduma.
Kwa upande wake, Rais Nandi-Ndaitwah amesema mafanikio ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Namibia hayatapimwa kwa makubaliano yaliyosainiwa, bali kwa uwekezaji, biashara na ajira zitakazotokana na ushiriki wa sekta binafsi.
Ametoa rai kwa sekta binafsi kutumia jukwaa hilo kugeuza fursa za Tanzania na Namibia kuwa uwekezaji, viwanda na ajira, huku ikijenga daraja jipya la biashara kati ya Afrika Mashariki na Kusini.
“Tuhame kutoka fursa kwenda uzalishaji, kutoka majadiliano kwenda vitendo, na kujenga ushirikiano utakaoleta ajira na maendeleo kwa watu wetu,” amesema Rais Nandi-Ndaitwah.























