NA GODFREY NNKO
WAKILI wa Serikali Mkoa wa Dar es Salaam, Domina Madeli amesema,Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeandaa Awamu ya Tatu ya Mafunzo Maalum ya Bespoke kwa Mawakili wa Serikali yenye lengo la kuwaimarisha kitaaluma ili waweze kuchangia ipasavyo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kusimamia kwa ufanisi masuala ya kisheria yanayohusiana na maendeleo ya nchi.
Madeli ameyabainisha hayo Juni 23,2026 katika kipindi maalum cha Twende Pamoja cha runinga ya Chanel Ten jijini Dae es Salaam wakati akizungumzia kuhusu maandalizi ya mafunzo hayo.
Amesema,Bespoke ni mafunzo yaliyosanifiwa mahsusi kwa ajili ya kukidhi mahitaji na malengo fulani ya kitaaluma,tofauti na mafunzo ya kawaida yanayotoa maarifa ya jumla kwa washiriki.
Amefafanua kuwa, dhana ya Bespoke inamaanisha mafunzo yanayotengenezwa kwa kuzingatia changamoto, mahitaji na majukumu maalum ya kundi husika, hivyo kulenga kutoa suluhisho la moja kwa moja kwa masuala yanayowakabili mawakili wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Bespoke ni mafunzo yaliyoundwa mahsusi kwa ajili ya kutatua au kulenga jambo fulani. Kama ilivyo kwa nguo inayoshonwa kwa vipimo vya mtu mmoja badala ya kununuliwa dukani, ndivyo ilivyo kwa mafunzo haya.Hayatoi maarifa kwa ujumla wake bali yanalenga eneo maalum la utendaji wa kazi,” amesema Madeli.
Amebainisha kuwa, tofauti na shahada ya sheria ambayo humwandaa mwanafunzi katika nyanja mbalimbali za taaluma ya sheria, mafunzo hayo yamekusudiwa kujikita katika maeneo mahususi yanayohitajika kwa wakati husika ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Kwa mujibu wa Madeli, mafunzo hayo ya Awamu ya Tatu ni mwendelezo wa programu iliyoanza mwaka 2024 na kuendelea mwaka 2025, huku awamu ya mwaka 2026 ikitarajiwa kufanyika kuanzia Julai 15 hadi 17 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (Arusha International Conference Centre (AICC).
Amesema,mafunzo hayo yanawahusu mawakili wote wa Serikali nchini na kwamba kila mmoja anahimizwa kushiriki ili kupata maarifa yatakayowasaidia kukabiliana na mahitaji mapya ya kisheria yanayoibuka katika mazingira ya sasa ya maendeleo.
Madeli amesema,wakati wa sasa ni muhimu kwa mafunzo hayo kutokana na Tanzania kuingia katika hatua mpya ya maendeleo kufuatia uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inaweka mwelekeo wa maendeleo ya muda mrefu ya taifa katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kimazingira.
Ameeleza kuwa,utekelezaji wa dira yoyote ya maendeleo hauwezi kufanikiwa bila kuwa na msingi imara wa kisheria unaounga mkono utekelezaji wake, jambo linalowapa mawakili wa Serikali nafasi muhimu katika kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
“Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inahitaji mifumo madhubuti ya sheria ili iweze kutekelezwa kwa mafanikio. Msingi wa uchumi shindani na shirikishi hauwezi kufikiwa bila uwepo wa wataalamu wa sheria wanaoelewa mazingira ya sasa ya maendeleo na wenye uwezo wa kushauri Serikali kwa weledi,” amesema.
Ameongeza kuwa,mawakili wa Serikali wanapaswa kuelewa mabadiliko yanayoendelea duniani, ikiwemo ushindani wa kiuchumi wa kimataifa, athari za mabadiliko ya tabianchi na mahitaji ya kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Kwa mujibu wa Madeli, mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo mawakili hao kutafsiri mabadiliko hayo katika mfumo wa sheria na sera ili kuhakikisha Tanzania inanufaika na fursa zilizopo huku ikikabiliana na changamoto zinazojitokeza.
Amesema,taifa lenye wananchi wenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi, kijamii na kisheria huwa na msingi imara wa maendeleo endelevu, na kwamba mafanikio hayo hayawezi kupatikana bila uwepo wa usimamizi madhubuti wa sheria.
“Ndiyo maana mafunzo haya ni muhimu katika kumuandaa mwanasheria wa Serikali kuwa mshauri na kiongozi wa masuala ya sheria atakayechangia kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,”amesema.
Akizungumzia mafanikio ya mafunzo hayo tangu kuanzishwa kwake, Madeli amesema yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uwezo wa mawakili wa Serikali katika kusimamia mikataba mikubwa ya uwekezaji na miradi ya kimkakati ya maendeleo.
Amesema ongezeko la miradi mikubwa inayotekelezwa kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) limeongeza umuhimu wa kuwa na mawakili waliobobea katika sheria za uwekezaji, biashara na mikataba ili kulinda maslahi ya taifa.
Kwa mujibu wa Madeli, sheria za ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ni eneo ambalo limeendelea kukua kwa kasi katika miaka ya karibuni, hivyo linahitaji wataalamu wenye uelewa wa kina ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo unafanyika bila vikwazo vya kisheria.
Ameonya kuwa,dosari ndogo katika uandishi au usimamizi wa mikataba mikubwa inaweza kusababisha ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi kwa miaka mingi, jambo linaloweza kuathiri maendeleo ya taifa na maslahi ya wananchi.
“Kwa sasa tunaona matokeo ya uwekezaji katika mafunzo haya. Miradi mingi ya kimkakati inaendelea kutekelezwa kwa mafanikio kutokana na uwepo wa mawakili wa Serikali wenye uwezo wa kusimamia mikataba na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wakati,” amesema.
Aidha, amesema maboresho ya sheria pamoja na kuongezeka kwa uwezo wa wataalamu wa sheria ndani ya Serikali yamechangia kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini, hali ambayo imeongeza imani kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Amesema tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo baadhi ya wawekezaji walikuwa na wasiwasi kuingia katika miradi ya ubia na Serikali, kwa sasa mazingira yameboreshwa na mfumo wa sheria umeimarishwa kiasi cha kuvutia uwekezaji zaidi.
“Hivi sasa wawekezaji wanaonesha imani kubwa katika mikataba ya ubia kwa sababu sheria zinasimamiwa kwa weledi, zimeboreshwa na zinaungwa mkono na wataalamu wa Serikali wenye uwezo wa kutosha kusimamia utekelezaji wake,”amesema.
Madeli amefafanua kuwa,mafunzo hayo yameandaliwa mahsusi kwa mawakili wa Serikali kutokana na jukumu lao katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali na kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa hatua hiyo haimaanishi kuwabagua mawakili wa sekta binafsi, bali ni kutokana na ukweli kwamba mafunzo hayo yamebuniwa kwa kuzingatia majukumu na mahitaji maalum ya mawakili wa Serikali katika kipindi hiki cha utekelezaji wa ajenda za maendeleo ya taifa.
“Mafunzo haya yameundwa mahsusi kwa kundi hili kwa sababu yana malengo ya moja kwa moja yanayohusiana na utekelezaji wa majukumu ya Serikali na kufanikisha maono ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050,”amesisitiza.