Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yahitimisha Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 kwa kusogeza huduma karibu na wananchi

DODOMA-Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imehitimisha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali za kisheria kwa wananchi waliotembelea banda la Ofisi katika Maadhimisho hayo yaliyoanza tarehe 16 hadi 23 Juni, 2026 katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yamehitimishwa tarehe 23 Juni, 2026 ambapo mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki S. Shemdoe ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt.Moses M.Kasiluka.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha Maadhimisho hayo, Prof. Shemdoe amewataka Watumishi wa Umma kuendelea kufanya kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa na kutoa huduma bora kwa wananchi.
"Niwaase Watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea tabasamu watanzania,"amesema Prof. Shemdoe.

Viongozi mbalimbali wa Serikali wametembelea banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na kupata maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na Ofisi katika Maadhimisho hayo, viongozi hao ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Prof. Godwin W. Kahyarara, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Franklin J. Rwezimula na Niabu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dr. Maduhu I. Kazi.

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeyatumia maadhimisho hayo katika kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi kwa kutoa huduma ya elimu na ushauri wa kisheria, utatuzi wa changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wananchi.

Akizungumza wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Wakili wa Serikali Mkuu,Bi.Happiness Nyabunya amewapongeza na kuwashukuru wananchi waliotembelea katika banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kupata elimu na ushauri wa kisheria.

“Tunawapongeza wananchi waliotenga muda wao na kuja kututembelea kwenye banda letu tunaamini elimu na ushauri tuliowapatia utakuwa umeongeza uelewa wao wa masuala ya kisheria,"amesema Bi.Happiness.
Aidha, Bi.Happiness ameeleza baadhi ya changamoto za kisheria zilizowasilishwa na wananchi katika banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa maadhimisho hayo zilihusu masuala ya ardhi, mirathi na masuala ya kifamilia.

Kwa upande wake, Bi. Emiliana Ibrahim ameridhishwa na kufurahishwa na elimu ya kisheria aliyoipata huku akifurahishwa na ufafanuzi wa kina kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisheria alioupata baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Nimefurahishwa na elimu niliyoipata, nimepokelewa vizuri na kueleweshwa hasa majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nimeondoka nikiwa na uelewa mpana sana wa jinsi ofisi hii inavyofanya,"amesema Bi. Emaculata.
Ushiriki wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni mojawapo ya jitihada za Ofisi katika kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here