Mbolea nchini ipo ya kutosha-Waziri Chongolo

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imewahakikishia wakulima uwepo wa mbolea ya kutosha nchini na itahakikisha inapatikana msimu wote ili waweze kuzalisha mazao ya kutosha.
Hayo yamesemwa leo Juni 3,2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Daniel Chongolo baada ya kufanya ziara ya kukagua maghala ya mbolea ya waagizaji,wazalishaji na wasambazaji wakubwa ikiwemo Kampuni ya ETG,Yara na OCP.

Amesema, lengo la ziara yake hiyo ni kujiridhisha kama uwepo wa mbolea upo sawa, ambapo ameshuhudia hifadhi kubwa ya mbolea huku ikiendelea kupakiwa kwa ajili ya kusambazwa kwenda maeneo ya mikoa mbalimbali nchini.
“Kwa hiyo, kwanza tumekuja kuwathibitishia wananchi na watanzania kwamba hofu kwamba labda mbolea hamna hayo yalikuwa mashaka tu na yasiyo na sababu.Mbolea nchini ipo, na sasa hivi tupo low season ya kilimo na ndiyo tunafika mwisho, maeneo makubwa ambayo yanaendesha kilimo kwa sasa ndiyo yapo kwenye mavuno.

“Lakini, yako maeneo kama ya Kilimanjaro, Arusha na sehemu za Manyara sasa hivi wako katikati ya msimu wa kilimo na tumefuatilia kujiridhisha kule mbolea inayohitajika zaidi ni Urea kwa ajili ya kukuzia,hapa wamesema wenyewe na mmesikia mbolea ipo na leo wametoa gari mbili zimepeleka mbolea Kilimanjaro.”

Waziri Chongolo amewahakikishia wananchi kuwa, mbolea ya kutosha kwa ajili ya hatua zote za kilimo nchini ipo ya kutosha na wataendelea kuhakikisha msimu wote wa kilimo inapatikana.

Vilevile amesema kuwa, Serikali itaendelea kutoa mbolea ya ruzuku kwa sababu kumekuwa na changamoto huko duniani ambayo imeathiri mifumo ya usambazaji huku ikiathiri mataifa mengi.

Amesema, maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wakulima hawakosi pembejeo na hilo wanalisimamia na kulitekeleza kwa ufanisi mkubwa kote nchini.
Pia, amesema waagizaji zaidi ya 18 wa mbolea nchini wana hifadhi ya kutosha ambayo inatoa uhakika wa mbolea ya kutosha hapa nchini.

Waziri Chongolo, pia amewaomba wakulima nchini kuwa watulivu kwani tayari Wizara ya Kilimo imepeleka timu nchi nzima ambayo inafanya tathimini ya mbolea iliyopo kwa kuwa, ipo ambayo ilikuja msimu uliopita na ikabaki huko kwa wasambazaji wadogo hivyo timu hiyo inaenda kujiridhisha ili kupata picha pana ya kisekta kuhusu akiba iliyopo, ipo sehemu gani na kama mkulima akiuliza aende kwa nani aweze kuipata.

Joel Laurent

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TFRA,Bw.Joel Laurent amesema kuwa,ETG ni miongoni mwa waagizaji wakubwa wa mbolea nchini ambapo baada ya kutembelea maghala ya kampuni hiyo na Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Daniel Chongolo wamejiridhisha kuhusu uwepo wa kutosha wa mbolea za aina zote.

“Tuwape uhakika wakulima wetu kwamba sasa, pamoja na kwamba tupo katika msimu unaoelekea kuisha, lakini mbolea zipo. Mbolea za kupandia, mbolea za kukuzia na hata kukaushia, unajua kuna wakulima ambao wana skimu za umwagiliaji kwa hiyo wanahitaji mbolea karibu misimu yote.”

Amesema,mbolea zilizopo nchini kwa sasa ni zaidi ya 180,000 huku kampuni hiyo na wengine wakiwa na mpango wa kuagiza mbolea kwa mwezi huu tu zaidi ya tani 68,000 huku miezi mitatu ijayo wakitarajia kuingiza nchini zaidi ya tani 320,000 za mbolea.

“Kwa hiyo ukiongeza na zile tani zilizopo ambazo zinaendelea kutumika, tunatoa uhakika kwamba mbolea itakuwepo na sisi kama Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania, tutahakikisha tunasimamia kuhakikisha wale waagizaji na wazalishaji ambao wamepanga kuleta au kuzalisha wanafanya hivyo ili tuweze kuhakikisha mbolea zinapatikana kabla ya msimu kuanza ambao unaanza mwezi wa tisa au mwezi wa 11.”

Kampuni ya ETG

Ranjeet Kumar ambaye ni Mkurugenzi wa Usambazaji wa Kampuni ya ETG amesema, kwa sasa wana hifadhi ya mbolea aina zote zaidi ya tani 47,000 huku wakitarajia kupokea tani 65,000 za UREA mwishoni mwa mwezi huu.
Amesema, licha ya changamoto mbalimbali zinazoendelea duniani ikiwemo vita katika Mashariki ya Kati, bado wamedhamiria kuhakikisha mbolea zote ziaendelea kupatikana na kuanzia sasa hadi mwezi Agosti, mwaka huu mbolea zote zinapatikana kwao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here