GEITA-Mkurugenzi na mmiliki wa Kadama English Medium Primary School Leticia Pastory ametunukiwa tuzo ya Mmiliki Bora wa Shule wa Kike Mkoa wa Geita 2026 (CEO Bora) ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuendeleza sekta ya elimu na maendeleo ya jamii.
Mwenyekiti wa UWT,Mary Chatanda akiwa na Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shilega, Mbunge wa Jimbo la Geita mjini Chacha Wambura na Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Geita Lorensia Bukwimba pamoja na Mkurugenzi wa Geita Women and Youth Foundation Cecylia Miraji wakati wa kukabidhi tuzo ya mmiliki bora wa shule mkoa wa Geita.
Mwenyekiti wa UWT Taifa,Mary Chatanda akimkabidhi tuzo ya Mmilki bora wa shule mkoa wa Geita Mkurugenzi wa Kadama English Medium Primary School,Leticia Pastory.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa Juni 6, 2026 na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa katika Tamasha la Mwanamke wa Dhahabu (Geita Women Festival 2026) lililofanyika katika Ukumbi wa Golden Social Hall mjini Geita.
Tuzo hizo zimeandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Geita Women and Youth Foundation chini ya Mkurugenzi wake Cecylia Miraji, kwa lengo la kutambua wanawake wenye mchango mkubwa na chanya katika jamii kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mkurugenzi wa shule za Waja na Mbunge wa jimbo la Geita Mjini,Chacha Wambura akimpongeza Mkurugenzi wa Kadama English Medium Primary School, Leticia Pastory kwa kushinda tuzo ya mmilki bora wa shule mkoa wa Geita 2026.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na jamii akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Geita,Martine Shigela, Mbunge wa Geita Mjini Chacha Wambura pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi.Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Leticia alisema heshima hiyo ni matokeo ya juhudi za muda mrefu za kuinua kiwango cha elimu katika Mkoa wa Geita kupitia Kadama English Medium Primary School.
Alisema shule hiyo imeendelea kufanya vizuri kitaaluma na kujijengea sifa ndani na nje ya mkoa kutokana na ubora wa ufundishaji na mazingira bora ya kujifunzia.
Miongoni mwa mafanikio makubwa ya shule hiyo ni mwaka 2018 ilipotoa mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa na mwingine aliyeshika nafasi ya pili kitaifa katika matokeo ya elimu ya msingi hatua iliyochangia kuitangaza shule hiyo kwenye ramani ya elimu nchini.
Leticia amesema tuzo hiyo itakuwa chachu ya kuendelea kuimarisha ubora wa elimu na kuwahamasisha wanawake wengine kutumia nafasi walizonazo kuleta maendeleo katika jamii.
"Tuzo hii ni motisha kwangu na kwa timu nzima ya Kadama English Medium Primary School kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi katika kuboresha elimu na malezi ya watoto wetu,"amesema.







