NA DIRAMAKINI
MWENYEKITI wa Kijiji cha Kisangara wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro amelazimika kurejesha pikipiki iliyokuwa imenunuliwa kwa fedha za msaada wa maendeleo ya kijiji baada ya uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kubaini kuwa mali hiyo ilisajiliwa kwa jina lake binafsi kinyume na kusudio la awali la wafadhili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro, Sabas Salehe, ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Mwanga ilipokea taarifa Mei 23, 2026 kutoka kwa mtoa taarifa aliyedai kuwa,mwaka 2025 Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisangara, Bw. Brayson Laurent Msofe aliomba msaada wa kununua pikipiki kwa ajili ya shughuli za ofisi ya kijiji.
Ilielezwa kuwa, mwenyekiti huyo aliwasilisha ombi hilo akidai kuwa umbali kati ya makazi yake na ofisi ya kijiji pamoja na mahitaji ya kuwafikia wananchi walioko katika vitongoji mbalimbali ulimlazimu kuwa na chombo cha usafiri ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kutokana na maombi hayo, Julai 15, 2025, mtoa taarifa alitoa kiasi cha Shilingi milioni 2.8 ambazo ziliwekwa katika akaunti ya benki ya Kijiji cha Kisangara iliyopo NMB Bank, kwa lengo la kununua pikipiki ya matumizi ya kijiji.
Hata hivyo, uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kuwa fedha hizo zilitumika kununua pikipiki mnamo Oktoba 17, 2025, lakini badala ya kusajiliwa kama mali ya kijiji, ilisajiliwa kwa jina binafsi la mwenyekiti huyo.
Aidha, pikipiki hiyo ilipewa namba ya usajili MC 266 FGQ huku mmiliki akionyeshwa kuwa ni Bw.Brayson Laurent Msofe.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa,hatua hiyo ilikuwa kinyume na makubaliano na malengo yaliyowasilishwa wakati wa kuomba msaada huo, jambo lililoibua tuhuma za kujinufaisha kwa kutumia mali iliyopaswa kuwa ya umma.
Baada ya kuitwa na kuhojiwa na TAKUKURU, mwenyekiti huyo alikiri kununua na kusajili pikipiki hiyo kwa jina lake binafsi.
Pia alieleza kuwa, tayari alikuwa ameshaiuza pikipiki hiyo, lakini alikubali kuwa kitendo hicho kilikuwa kosa na akaonesha utayari wa kurejesha mali ya kijiji.
Kutokana na hatua hiyo, Juni 8,2026, Bw. Msofe aliambatana na viongozi wa Halmashauri ya Kijiji pamoja na Mtendaji wa Kijiji cha Kisangara kwenda Moshi kwa ajili ya kununua pikipiki mpya ambayo ilikabidhiwa na kuhifadhiwa katika ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro kabla ya kukabidhiwa rasmi kwa matumizi ya kijiji.
Sabas Salehe alisema,tukio hilo linapaswa kuwa fundisho kwa viongozi wote wanaosimamia rasilimali za umma kuwa waaminifu na waadilifu katika matumizi ya mali zinazotolewa kwa manufaa ya wananchi.
“Viongozi wote waliopewa dhamana ya kulinda mali za umma wanapaswa kuhakikisha mali hizo zinatumika kwa maslahi ya wananchi. Kinyume chake, wanaweza kujikuta wakikabiliwa na hatua za kisheria kutokana na makosa ya rushwa au matumizi mabaya ya mali za umma."
TAKUKURU imeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa taarifa za vitendo vinavyohatarisha matumizi sahihi ya mali za umma ili kuhakikisha uwajibikaji, uwazi na maendeleo endelevu katika jamii.
Aidha, kauli mbiu ya taasisi hiyo inaendelea kuwa: “Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu; Tutimize Wajibu Wetu.”
