NA DIRAMAKINI
MAHAKAMA ya Wilaya ya Iringa mkoani Iringa imemtia hatiani aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Muwimbi kilichopo Kata ya Lumuli, Wilaya ya Iringa mkoani Iringa, Rodeligo Kasian Mbwale baada ya kukiri kosa la kughushi saini ya Mtendaji wa Kijiji katika hati ya mauziano ya shamba.
Mfano wa saini, si ya Mwenyekiti husika. Picha na Mtandao.
Hukumu hiyo ilitolewa leo Juni 26,2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Mheshimiwa Rehema Mayagilo katika shauri la jinai namba 10615/2026 kati ya Jamhuri dhidi ya Rodeligo Kasian Mbwale.
Mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa baada ya kukiri kosa linalomkabili na kumhukumu kifungo cha nje cha miezi 12 pamoja na kulipa faini ya shilingi 800,000.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Mbwale alikuwa anakabiliwa na kosa moja la kughushi saini ya Mtendaji wa Kijiji cha Muwimbi, Bi. Mariam Mwakalinga katika hati ya mauziano ya shamba iliyohusisha mwananchi mmoja na raia wa kigeni mwenye asili ya China.
Inadaiwa kuwa, tukio hilo lilitokea Oktoba 1, 2025, ambapo mshtakiwa alighushi saini hiyo kwa lengo la kuhalalisha mchakato wa mauziano ya shamba bila idhini halali ya mtendaji husika.
Upande wa mashtaka uliendeshwa na Mawakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Salum Bhoki na Lisa Kasongwa ambao waliwasilisha ushahidi uliosababisha mshtakiwa kukiri kosa lake na kutiwa hatiani.
Aidha,hukumu hiyo inaendelea kutuma ujumbe kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria katika usimamizi wa nyaraka za umma na miamala ya ardhi, huku mamlaka zikisisitiza kuwa vitendo vya kughushi nyaraka na saini za watumishi wa umma vitaendelea kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
