NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) yenye lengo la kuwawezesha waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu kupata mafunzo ya ufundi stadi yatakayowawezesha kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa.
Makubaliano hayo yamesainiwa jijini Dar es Salaam leo Juni 4, 2026 katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa taasisi hizo pamoja na wadau mbalimbali ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha huduma za tiba, urejeshaji na uwezeshaji wa waraibu wa dawa za kulevya baada ya matibabu.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema, ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuhakikisha waraibu waliopata nafuu wanapatiwa fursa za kujenga maisha mapya na kuwa sehemu ya nguvu kazi yenye tija kwa maendeleo ya nchi.
Amesema,matumizi ya dawa za kulevya yameendelea kuwa changamoto kubwa inayozikabili jamii nyingi duniani, hususan kwa vijana ambao ndio tegemeo la maendeleo ya baadaye ya Taifa.
"Tatizo la dawa za kulevya halileti madhara ya kiafya pekee, bali pia huathiri uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia na Taifa kwa ujumla. Vilevile huchangia kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, migogoro ya kifamilia, kuporomoka kwa maadili na kupungua kwa nguvu kazi yenye tija,”amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Amefafanua kuwa,Serikali kupitia DCEA imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya ikiwemo kuzuia biashara haramu ya dawa hizo, kutoa elimu kwa umma pamoja na kuimarisha huduma za tiba na urejeshaji kwa waraibu.
Hata hivyo, amesema uzoefu unaonesha kuwa, matibabu pekee hayatoshi iwapo waraibu waliopona hawatapewa fursa za kujiendeleza kiuchumi na kijamii.
“Watu wengi wanaopata nafuu kutokana na uraibu hukabiliwa na changamoto za ukosefu wa ajira, kipato na wakati mwingine kunyanyapaliwa na jamii. Hali hiyo inaweza kuwafanya kurejea tena katika matumizi ya dawa za kulevya. Ndiyo maana ushirikiano huu na VETA una umuhimu mkubwa,”amesisitiza.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, waraibu waliopona watapata nafasi ya kujiunga na vyuo vya VETA vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini kwa gharama nafuu ili kupata mafunzo katika fani mbalimbali za ufundi stadi ikiwemo ufundi seremala, umeme, ushonaji, ufundi magari,Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), upishi pamoja na taaluma nyingine zinazohitajika katika soko la ajira.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema,matarajio ya mpango huo ni kuhakikisha wahitimu wanapata uwezo wa kujiajiri na kujitegemea kupitia shughuli za uzalishaji mali baada ya kuhitimu mafunzo yao.
Aidha, amesema DCEA itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha zinazotoa mikopo midogo midogo ili kuwaunganisha wahitimu hao na fursa za mitaji zitakazowawezesha kuanzisha biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.
Ameongeza kuwa,mpango huo unatekeleza kwa vitendo dhana ya kuwapa wananchi nafasi ya pili katika maisha kwa kuwa waraibu waliopona wanahitaji kuungwa mkono, kuaminiwa na kupewa mazingira yatakayowawezesha kurejesha heshima na mchango wao katika jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore amesema,mamlaka hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa mafanikio ili kuwasaidia waraibu waliopata nafuu kupata ujuzi utakaowawezesha kushiriki katika shughuli za uzalishaji na maendeleo.
CPA Kasore amesema,VETA imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na ina jukumu la kuratibu, kugharamia na kutoa mafunzo ya ufundi stadi yanayolenga kukidhi mahitaji ya maendeleo ya jamii na soko la ajira.
Amesema,kwa sasa VETA ina vyuo 80 vinavyotoa mafunzo katika ngazi za mikoa na wilaya kote nchini, huku Serikali ikiendelea kupanua huduma hizo kupitia ujenzi wa vyuo vingine 64 katika wilaya mbalimbali pamoja na chuo kimoja cha Mkoa wa Songwe.
Pia,amebainisha kuwa,VETA imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi kupitia misaada ya vifaa, ufadhili wa masomo na mafunzo ya kuwajengea uwezo wakufunzi na wanafunzi.
“Leo ni siku muhimu kwa VETA na DCEA kwa sababu tunaanzisha ushirikiano utakaowasaidia vijana na wananchi waliowahi kuathirika na matumizi ya dawa za kulevya, lakini sasa wamepona na wako tayari kushiriki katika ujenzi wa Taifa. Kupitia mafunzo haya watapata fursa ya kuajiriwa,kujiajiri na hata kuajiri wengine,”amesema.
Ameongeza kuwa,VETA pia ipo tayari kuwasaidia waraibu waliowahi kupata ujuzi kupitia mfumo usio rasmi kwa kuwatathmini na kuwarasimishia ujuzi wao ili waweze kupata vyeti vinavyotambulika rasmi na kuongeza fursa zao katika soko la ajira.
CPA Kasore ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya elimu ya ufundi stadi na kuwezesha VETA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Aidha,ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuwahamasisha vijana kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi ili kujenga uwezo wa kujitegemea na kuepuka kujiingiza katika vitendo hatarishi ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya.
Ushirikiano kati ya DCEA na VETA ni hatua muhimu katika kuimarisha juhudi za Serikali za kukabiliana na athari za dawa za kulevya nchini kwa kuwajengea uwezo waraibu waliopata nafuu na kuwapa fursa ya kuanza maisha mapya yenye tija kwao binafsi,familia zao na Taifa kwa ujumla.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
VETA Tanzania








