DODOMA-Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Nhamanilo Kwagilwa, ameitaka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuendelea kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinawafikia wananchi wote, hususan wanaoishi katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mbali yanayokabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano.
Mhe. Kwagilwa ameyasema hayo alipotembelea banda la TMA wakati wa Ufunguzi wa Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 yanayofanyika kuanzia tarehe 1 hadi 5 Juni 2026 katika Viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre (JKCC), jijini Dodoma, chini ya kauli mbiu isemayo "Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania"
Akizungumza na wataalamu wa TMA, Mhe. Kwagilwa ameipongeza mamlaka hiyo kwa kazi kubwa inayoendelea kufanya katika utoaji wa huduma za hali ya hewa na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha taarifa hizo zinawafikia wananchi wanaozitegemea katika shughuli zao za kila siku, hususan sekta ya kilimo.
"Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya na tunaona matokeo yake. Hata hivyo, kuna umuhimu wa kuhakikisha taarifa hizi zinawafikia wananchi waliopo kwenye maeneo ya mbali ambao wanategemea utabiri wa hali ya hewa katika shughuli zao za kimsimu, hasa kilimo,” amesema Mhe. Kwagilwa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya TMA na Vituo vya Kijamii vya Uhimilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi (CCCRC) ili vituo hivyo viwe daraja muhimu la kufikisha taarifa za hali ya hewa kwa wananchi ngazi ya jamii na kuwawezesha kupata taarifa sahihi zinazohusu maeneo yao pamoja na mwongozo wa hatua stahiki za kuchukua katika misimu mbalimbali.
Ushiriki wa TMA katika maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za Mamlaka kuendelea kusogeza huduma za hali ya hewa kwa wananchi, kuongeza uelewa wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika sekta mbalimbali za maendeleo na kuimarisha ushirikiano na wadau.
TMA inawakaribisha wananchi, wadau wa mazingira, watafiti, wanafunzi na washiriki wote wa maonesho hayo kutembelea banda la TMA ili kujifunza zaidi kuhusu huduma za hali ya hewa na mifumo ya utoaji wa utabiri wa hali ya hewa.
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania



