Ni Bajeti Kuu ya kazi na utu,tunasonga mbele 2026/2027

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) leo Juni 11,2026 bungeni jijini Dodoma amewasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27, akisisitiza kuwa bajeti hiyo inalenga kujenga uchumi himilivu kupitia mageuzi ya kidijitali,uwekezaji wa kimkakati na sera endelevu za kifedha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akifuatilia Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/2027, kupitia Televisheni ya Taifa (TBC1), Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 11 Juni, 2026. Bajeti hiyo ilikuwa ikisomwa Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, kwenye Bunge la 13, Mkutano wa tatu katika Kikao cha 48 jijini Dodoma.
Bajeti hiyo ni ya kwanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwa pia imejengwa katika misingi ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa (2026/27–2030/31), Ilani ya CCM ya 2025, pamoja na ajenda za kikanda na kimataifa kama Dira ya EAC 2050 na Malengo Endelevu ya Maendeleo 2030.

Kwa mujibu wa hotuba hiyo, Serikali inalenga kukuza uchumi hadi kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026, huku mfumuko wa bei ukidhibitiwa kubaki kati ya asilimia 3 hadi 5.

Vilevile, mapato ya ndani yanatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 17.1 ya Pato la Taifa, huku nakisi ya bajeti ikipangwa kutokuzidi asilimia 3 ya Pato la Taifa. Akiba ya fedha za kigeni inatarajiwa kuendelea kukidhi uagizaji wa bidhaa kwa angalau miezi minne.

Pia,Serikali imesisitiza kujitegemea kifedha kutokana na kupungua kwa misaada ya kimataifa na changamoto za mikopo. Hatua mbalimbali zimewekwa, ambapo Waziri wa Fedha amesema ni pamoja na kuimarisha mifumo ya TEHAMA ya kodi,kupambana na mianya ya upotevu wa mapato,kupanua wigo wa kodi kupitia uwekezaji.
Vilevile, Serikali imedhamiria kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari,kuimarisha matumizi ya mashine za EFD, matumizi ya Akili Unde (AI) na Big Data

Waziri wa Fedha amesema,Serikali pia itaanzisha programu ya Tuzo ya Uzalendo kupitia mfumo wa risiti za kielektroniki ili kuongeza nidhamu ya kodi kwa wananchi na wafanyabiashara.

Amesema,bajeti mpya inalenga kuimarisha viwanda, hasa vinavyotegemea madini na nishati kama gesi asilia, chuma na makaa ya mawe. Miradi mikubwa ya miundombinu pia itaendelezwa, ikiwemo SGR na uhuishaji wa reli ya TAZARA.

Aidha, Serikali inapanga kuanzisha Dar es Salaam International Financial Centre (DIFC) ili kuvutia mitaji ya kimataifa.

Serikali imetangaza mpango wa kupunguza matumizi ya fedha taslimu kwa kuweka ulazima wa malipo ya kidijitali katika sekta mbalimbali zikiwemo usafiri wa mabasi, treni,vivuko na ndege.
Kwa upande wa elimu,biashara kubwa na masoko,utalii na hoteli ikiwemo kilimo kupitia vyama vya ushirika ambapo hatua hii inalenga kuongeza uwazi, kupunguza gharama na kudhibiti vitendo vya uvujaji wa fedha za umma,

Waziri wa Fedha, pia ameelezea mafanikio makubwa ya Serikali kupitia ukaguzi ambapo zaidi ya asilimia 98 ya taasisi za Serikali Kuu zilipata hati safi. Hata hivyo, changamoto bado zipo kwenye miradi kuchelewa na matumizi yasiyozingatia taratibu.

Miongoni mwa hatua ambazo zinatarajiwa kuchukuliwa ni kuunganisha mifumo yote ya fedha za umma,kupunguza safari na mikutano isiyo na tija, kuimarisha ukaguzi wa ndani,kudhibiti mikataba isiyoidhinishwa na Bunge ikiwemo kuimarisha usimamizi wa mali za umma

Serikali pia imeendelea kuimarisha mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia halmashauri, Mfuko wa Machinga na programu za uwezeshaji kiuchumi.

Pia, zaidi ya shilingi bilioni 135 zimetolewa kwa vikundi vya kijamii kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipiga makofi pamoja na Wasaidizi wake mara baada ya Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar kumaliza kuwasilisha Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/2027 kwenye Bunge la 13, Mkutano wa tatu katika Kikao cha 48 Jijini Dodoma. Rais Dkt. Samia alikuwa akifuatilia Hotuba ya Bajeti hiyo Kuu ya Serikali kupitia Televisheni ya Taifa (TBC1), Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 11 Juni, 2026.

Bajeti ya 2026/27 imeelezwa kuwa ni ya mageuzi makubwa yanayolenga kujenga uchumi wa kisasa, jumuishi na unaojitegemea, huku Serikali ikisisitiza nidhamu ya matumizi ya fedha, ukuaji wa viwanda na uimarishaji wa mifumo ya kidijitali.

Aidha,Serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inatarajiwa kuendelea kusimamia mageuzi ya kiuchumi kwa lengo la kufikia maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi wote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here