DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Mahakama ya Tanzania kuendelea kusimamia haki, nidhamu, uwajibikaji na maadili katika utoaji haki ili kuwa na mfumo imara wa utoaji haki nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akimuapisha Dkt. John Anthony Jingu kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 19 Juni, 2026.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo Ikulu Dar es Salaam, katika hafla ya kumuapisha Dkt. John Anthony Jingu kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Amesema Serikali itaendelea kuuwezesha Mhimili wa Mahakama kwa mifumo, miundombinu na rasilimali watu, akibainisha kuwa maboresho hayo tayari yameongeza ufanisi na kuboresha utoaji haki na huduma za Mahakama nchini.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amemtaka Dkt. Jingu kuendeleza kazi nzuri Iliyofanywa na mtangulizi wake, Prof. Elisante Ole Gabriel, ambaye amestaafu.
Amemshukuru Prof. Gabriel kwa kusimamia maboresho ya kiutendaji ndani ya Mahakama na kuacha msingi mzuri wa kuendelezwa.
Aidha, Rais Dkt. Samia amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju, kwa kuendelea kusimamia Mahakama kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili, hatua iliyosaidia kuimarisha utendaji na hadhi ya Mhimili huo katika mfumo wa haki nchini.
Vilevile, amewataka viongozi wa Mahakama nchini kuendelea kusimamia nidhamu na uwajibikaji ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati, kwa heshima na kwa mujibu wa sheria.
