NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kupokea gawio na michango mbalimbali kutoka kwa taasisi za umma pamoja na kampuni ambazo Serikali imewekeza. Ni katika hafla ya Siku ya Gawio 2026 itakayofanyika Juni 30, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo linaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuonesha mafanikio ya uwekezaji wa Serikali katika mashirika ya umma na kampuni zenye hisa za Serikali, huku likilenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na tija katika usimamizi wa rasilimali za umma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Juni 15, 2026, Naibu Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki amesema, kaulimbiu ya Siku ya Gawio mwaka huu ni “Uwekezaji wa Umma wenye Matokeo: Nguzo ya Uchumi Shindani na Maendeleo Endelevu kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.”
Amesema,kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza taasisi za umma kuongeza ufanisi, tija na uwajibikaji katika usimamizi wa mali za umma ili kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unaleta manufaa yanayoonekana kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Pia, amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwazi, uwajibikaji na usimamizi wa uwekezaji wa umma ili kuhakikisha rasilimali zilizowekezwa katika taasisi, mashirika ya umma na kampuni zenye hisa za Serikali zinaendelea kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Amebainisha kuwa,thamani ya uwekezaji wa Serikali katika taasisi, mashirika ya umma na kampuni zenye hisa za Serikali imefikia takribani shilingi trilioni 95, jambo linalodhihirisha ukubwa wa mtaji wa umma unaosimamiwa na umuhimu wa kuhakikisha uwekezaji huo unazalisha faida na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Bi.Mauki amesema,Siku ya Gawio imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kupima mafanikio ya uwekezaji wa Serikali kwa kutoa fursa ya kuonesha kiwango cha gawio na michango inayorejeshwa serikalini kutoka katika taasisi na mashirika mbalimbali.
Vilevile, ameeleza kuwa,kupitia jukwaa hilo, wananchi hupata nafasi ya kufahamu namna mali za umma zinavyosimamiwa, huku Serikali ikiongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi na usimamizi wa rasilimali za taifa.
Bi.Mauki amewapongeza viongozi wa taasisi na mashirika ambayo tayari yamekamilisha kuwasilisha gawio na michango yao serikalini, huku akizitaka taasisi ambazo bado hazijatimiza wajibu huo kuhakikisha zinakamilisha zoezi hilo kabla ya tarehe ya hafla hiyo.
Amesema,taasisi zitakazoonesha utendaji bora zaidi na kutoa gawio kubwa kwa Serikali zitatunukiwa tuzo maalum na Rais Dkt.Samia.
Naibu Msajili wa Hazina amesema,utaratibu huo unalenga kuhamasisha ushindani chanya, kuongeza uwajibikaji na kuimarisha utamaduni wa kufanya kazi kwa kuzingatia matokeo.
Amewataka Watanzania kutumia Siku ya Gawio 2026 kama fursa ya kutathmini matokeo ya uwekezaji wa Serikali na kuona namna rasilimali za taifa zinavyotumika kuleta maendeleo na ustawi kwao na Taifa kwa ujumla.
“Tunawashukuru sana waandishi wa habari kwa kuendelea kuitikia wito wetu na kuonesha thamani yenu kama wadau muhimu wa uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa uwekezaji wa Serikali. Kupitia kazi yenu, wananchi wanaendelea kupata taarifa sahihi kuhusu uwekezaji wa Serikali na matokeo yake."
Siku ya Gawio 2026 inatarajiwa kukutanisha viongozi wa Serikali, wakuu wa taasisi na mashirika ya umma, wadau wa sekta ya uwekezaji pamoja na wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha usimamizi wa mali za umma na kuhakikisha uwekezaji unaofanywa kwa niaba ya wananchi unachangia ukuaji wa uchumi shindani na maendeleo endelevu ya Tanzania kuelekea mwaka Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Aidha,gawio na michango inayotolewa na taasisi za umma ni moja ya vyanzo muhimu vya mapato yasiyo ya kodi kwa Serikali, hali inayosaidia kuongeza uwezo wa kugharamia huduma za kijamii na miradi ya maendeleo bila kuongeza mzigo wa kodi kwa wananchi.
Gawio Day 2025
Mwaka 2025,Serikali ilipokea gawio la jumla ya Shilingi Trilioni 1.028 kutoka katika Mashirika na Taasisi za Umma ikiwa ni ongezeko la asilimia 34 ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 767 zilizotolewa mwaka 2024.
Aidha, idadi ya Mashirika na Taasisi zilizochangia iliongeza kufikia 213, huku kampuni zenye hisa chache za Serikali zikiwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa, zikiwemo Twiga Minerals (Shilingi Bilioni 93.6), Airtel Tanzania (Shilingi Bilioni 73.9) na NMB Bank (Shilingi Bilioni 68.1).
