Kombe la Dunia 2026:Japan yailazimisha Uholanzi sare ya 2-2 katika mchezo wa kusisimua

NA DIRAMAKINI

TIMU ya Taifa ya Japan imeonesha moyo wa kupambana kwa dakika zote 90 baada ya kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Uholanzi katika mchezo wa Kundi F wa Kombe la Dunia 2026. Mtanange huo umepigwa leo katika Uwanja wa AT&T, Texas nchini Marekani.
Mchezo huo uliokuwa wa kusisimua ulianza kwa tahadhari kubwa kutoka kwa pande zote mbili kabla ya kipindi cha pili kushuhudia mvua ya mabao manne yaliyowafanya mashabiki kushuhudia moja ya mechi bora zaidi za hatua ya makundi hadi sasa.

Nahodha wa Uholanzi, Virgil van Dijk, aliifungia timu yake bao la kwanza dakika ya 51 kwa kichwa maridadi na kuwapa Waholanzi matumaini ya kuanza kampeni yao kwa ushindi.

Hata hivyo, Japan haikukata tamaa na ilijibu haraka dakika ya 57 kupitia Keito Nakamura aliyesawazisha matokeo na kuamsha matumaini ya mashabiki wa Samurai Blue.

Uholanzi walirejesha uongozi dakika ya 64 kupitia Crysencio Summerville aliyefunga bao zuri lililoonekana kuisogeza timu yake karibu na ushindi muhimu wa kwanza wa kundi hilo.

Hata hivyo, Japan waliendelea kushinikiza na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 88 wakati Daichi Kamada alipofunga bao la kusawazisha na kuinyima Uholanzi ushindi waliokuwa wameusogelea kwa muda mrefu.

Matokeo hayo yanalifanya Kundi F kuendelea kuwa wazi huku timu zote zikibakiwa na nafasi ya kupigania kufuzu hatua inayofuata.

Uholanzi sasa wataelekeza nguvu zao kwenye mchezo dhidi ya Sweden, wakati Japan wakijiandaa kuvaana na Tunisia katika mechi zao zijazo.

Aidha,sare hiyo imeonekana kuwa ushindi mkubwa kwa Japan waliorejea mara mbili kusawazisha matokeo dhidi ya moja ya timu zenye uzoefu mkubwa katika michuano hiyo, huku Uholanzi wakibaki na maswali kuhusu uwezo wao wa kulinda uongozi katika mechi muhimu za mashindano hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here