DODOMA-Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) zimekubaliana kuharakisha hatua za kukamilisha mikataba ya ufadhili wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa Jiji la Mwanza Awamu ya Pili (LV WATSAN II), unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo jirani.
Hayo yamejiri jijini Dodoma baada ya Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule, kwa niaba ya Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Dkt. Natu E-maamry Mwamba alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) ulioongozwa na Mkuu wa Kitengo kinachoratibu Mahusiano ya Nchi na Sekta ya Umma kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Bw. Christian Elias.
Mazungumzo hayo yametoa fursa kwa pande zote mbili kufanya tathmini ya ushirikiano uliopo na kubaini maeneo mapya ya ushirikiano yatakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Katika kikao hicho, pande zote zimejadili maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea nchini kupitia ufadhili wa Benki hiyo pamoja na fursa za ufadhili wa miradi mipya katika sekta za maji na usafiri, ambazo ni muhimu katika kuboresha huduma za kijamii na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aidha, pande hizo zimejadili hatua za mwisho za kukamilisha mkataba wa ufadhili wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka wa Dar es Salaam Awamu ya Nne na Tano (BRT IV & V), unaotarajiwa kuimarisha huduma za usafiri wa umma na kupunguza changamoto za msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.
Mbali na Sekta za Maji na Usafiri, mazungumzo hayo yamegusia maeneo mengine ya kipaumbele kwa maendeleo ya Taifa, ikiwemo miradi ya nishati, mawasiliano na ya habari na (TEHAMA), pamoja na programu za uwezeshaji wa wajasiriamali kupitia mikopo inayotolewa EIB kwa benki za biashara hapa nchini.
Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule amesema,Serikali inathamini mchango wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) katika kusukuma mbele ajenda za maendeleo nchini.
“Ushirikiano huu ni muhimu katika kuharakisha utekelezaji wa miradi na programu zinazochangia maendeleo endelevu ya nchi yetu,”amesema Bw. Mtengule.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo kinachoratibu Mahusiano ya Nchi na Sekta ya Umma kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), Bw. Christian Elias ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa mapokezi mazuri pamoja na ushirikiano unaotolewa na timu ya wataalamu katika kuendeleza ajenda hizo muhimu.
“Tunatazamia kukamilisha hatua zinazofuata, ikiwemo kusainiwa kwa mikataba ya ufadhili ya miradi ya BRT IV & V na LV WATSAN na kuanza utekelezaji wa miradi hhiyo"amesema Bw. Elias.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Bajeti, Bi. Vicky Jengo; Kaimu Kamishna Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Madeni, Bw. Mulesi Manyama; Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, Bw. Jonathan Mpuya; pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (EIB).

