NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Mashariki mwa Libya yenye makao yake mjini Benghazi imetangaza kupiga marufuku raia wa nchi nne za Afrika kuingia katika maeneo inayoyasimamia, ikieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kuimarisha na kupanga upya mfumo wa udhibiti wa wageni wanaoingia nchini humo.
Osama Hamad.(Picha na Mtandao).
Kwa mujibu wa tamko lililotolewa Jumanne na serikali hiyo, raia wa Sudan, Eritrea, Ethiopia na Somalia hawataruhusiwa kuingia katika maeneo yanayodhibitiwa na utawala wa Benghazi kupitia mipaka ya nchi kavu, baharini au viwanja vya ndege.
Serikali hiyo inaongozwa na Osama Hamad na inaungwa mkono na Kamanda wa Jeshi la Taifa la Libya, Khalifa Haftar ambaye anadhibiti sehemu kubwa ya Mashariki na Kusini mwa nchi hiyo.
Chanzo kutoka serikalini kilinukuliwa kikisema kuwa, uamuzi huo haujalenga taifa lolote mahususi bali unakusudia kupanga upya utaratibu wa kuingia kwa raia wa kigeni katika maeneo yanayosimamiwa na serikali hiyo.
Hata hivyo, marufuku hiyo haitawahusu wanadiplomasia na maafisa wa balozi kutoka nchi hizo nne pamoja na familia zao, mradi wawe wametambuliwa rasmi na mamlaka husika.
Vilevile, serikali hiyo imetoa msamaha kwa wataalamu wanaofanya kazi katika sekta za elimu, afya na huduma nyingine zinazohusiana na afya, ikiwa watakuwa na vibali vinavyotakiwa pamoja na mikataba halali ya ajira iliyoidhinishwa na mamlaka husika.
Kwa sasa Libya ina tawala mbili zinazoshindania uongozi wa nchi hiyo. Serikali inayotambulika kimataifa inaongozwa na Abdulhamid Dbeibah yenye makao yake mjini Tripoli, ambayo iliundwa mwaka 2021 kupitia mchakato ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Tangu kuanguka kwa utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011 kufuatia uasi ulioungwa mkono na NATO, Libya imeendelea kukabiliwa na migogoro ya kisiasa na kiusalama iliyogawanya nchi katika maeneo yanayodhibitiwa na makundi tofauti ya kisiasa na kijeshi.
Kutokana na hali hiyo, Libya imeendelea kuwa mojawapo ya njia kuu zinazotumiwa na wahamiaji kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wanaokimbia vita, umaskini na ukosefu wa fursa za kiuchumi wakielekea barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania.
Uamuzi huo unatarajiwa kuwa na athari katika mwenendo wa uhamiaji na usafiri wa raia kutoka nchi hizo nne, huku ukizua mjadala kuhusu sera za uhamiaji na usalama katika taifa hilo ambalo bado linakabiliwa na changamoto za kisiasa na kiusalama.(Reuters)
