Serikali yawahakikishia wakulima mbolea ya kutosha Msimu wa 2026/27, bei za Dunia zaonesha kushuka

NA GODFREY NNKO

WAKATI maandalizi ya msimu mpya wa kilimo wa 2026/2027 yakishika kasi nchini, Serikali imewahakikishia wakulima kuwa hakuna sababu ya kuwa na hofu kuhusu upatikanaji wa mbolea, ikieleza kuwa taifa lina akiba ya kutosha pamoja na mpango madhubuti wa kuongeza shehena mpya za pembejeo hizo muhimu kabla ya kuanza kwa msimu mkuu wa uzalishaji.
Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Daniel Chongolo baada ya kufanya ziara Juni 3,2026 ya ukaguzi katika maghala ya waagizaji wakubwa wa mbolea jijini Dar es Salaam, ambapo alijionea hali ya akiba iliyopo na mipango ya usambazaji kuelekea msimu ujao wa kilimo.

Hatua hiyo inakuja katika kipindi ambacho dunia imeendelea kushuhudia misukosuko katika biashara ya pembejeo za kilimo kutokana na migogoro ya kimataifa, hususan vita vinavyoendelea katika Mashariki ya Kati ambavyo vimeathiri usafirishaji wa bidhaa mbalimbali duniani.

Utoshelevu na asilimia 20 ziada

Takwimu za Wizara ya Kilimo zinaonesha kuwa hadi Mei 31, 2026, jumla ya tani 1,301,410 za mbolea zilikuwa zimeingizwa nchini, kiwango kinachozidi mahitaji ya msimu wa 2025/2026 yaliyokadiriwa kuwa tani 1,084,000.

Hali hiyo ina maana kuwa upatikanaji wa mbolea umefikia asilimia 120 ya mahitaji yote ya msimu uliomalizika, jambo linaloonesha mafanikio ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha pembejeo hizo muhimu zinapatikana kwa wakati.

Katika kiasi hicho, tani 1,099,325 tayari zimeuzwa na kutumiwa na wakulima katika maeneo mbalimbali nchini, huku tani 187,149 zikiendelea kuhifadhiwa kwenye maghala kama akiba ya taifa.

Wataalamu wa sekta ya kilimo wanaeleza kuwa, kiwango hicho cha akiba ni muhimu katika kuhakikisha hakuna upungufu wa mbolea wakati wa kipindi cha mpito kati ya msimu mmoja na mwingine, hususan kwa wakulima wanaotumia mifumo ya umwagiliaji ambao huendelea na uzalishaji mwaka mzima.

Shehena mpya mbioni

Mbali na akiba iliyopo, Serikali imetangaza kuwa tani 68,000 za mbolea aina ya DAP, Urea na CAN zinatarajiwa kuwasili nchini kabla ya mwisho wa Juni,2026.

Mbolea hizo zinaagizwa na kampuni kubwa za ETG, Yara na TFC ambazo ni miongoni mwa wadau wakuu wa usambazaji wa pembejeo nchini.

Aidha, katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu, tani nyingine 387,236 zinatarajiwa kuingizwa nchini ili kujiandaa na mahitaji ya msimu mpya wa kilimo.

Kwa mujibu wa mpango wa Serikali, mahitaji ya mbolea kwa msimu wa 2026/2027 yanakadiriwa kufikia tani 1.2 milioni, huku lengo likiwa ni kuhakikisha tani 1.5 milioni zinapatikana kwa ajili ya wakulima.

Kati ya kiasi hicho, tani milioni 1.1 zitaagizwa kutoka nje ya nchi na tani 400,000 zitazalishwa na viwanda vya ndani.

Nafuu bei ya Dunia

Habari njema kwa wakulima ni kwamba baada ya miezi kadhaa ya kupanda kwa kasi, bei za mbolea katika soko la dunia zimeanza kuonesha dalili za kushuka.

Takwimu zinaonesha kuwa,bei ya mbolea ya Urea ilishuka kutoka dola za Marekani 943 kwa tani mwezi Aprili hadi dola 658 mwishoni mwa Mei, sawa na punguzo la karibu asilimia 29.

Mbolea ya DAP nayo imeonesha mwenendo wa kushuka kwa takribani asilimia 34, huku CAN na NPK 17:17:17 zikishuka kwa asilimia 43 na 27 mtawalia.

Wataalamu wanaeleza kuwa,kushuka kwa bei hizo kunachangiwa na kupungua kwa gharama za gesi asilia ambayo ndiyo malighafi kuu inayotumika kuzalisha mbolea nyingi za Nitrojeni duniani.

Pia, kuimarika kwa minyororo ya usambazaji na kuongezeka kwa uzalishaji katika baadhi ya nchi zinazozalisha mbolea kwa wingi kumechangia kurejea kwa utulivu katika soko la kimataifa.

Ruzuku ya Mbolea

Pamoja na dalili za kushuka kwa bei duniani, Serikali imeeleza kuwa itaendelea na utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku ya Mbolea ili kuhakikisha wakulima wanaendelea kupata pembejeo kwa gharama nafuu.

Waziri Chongolo amesema,Serikali inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wakulima hawakosi pembejeo muhimu kwa uzalishaji wa mazao.

Amesema,ruzuku hiyo itaendelea kutolewa hadi pale bei za mbolea zitakapokuwa himilivu vya kutosha katika soko la dunia na ndani ya nchi.

Hatua hiyo inaonekana kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, hasa katika kipindi ambacho dunia bado inakabiliwa na changamoto za kiuchumi na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kampeni ya "Mali Shambani, Silaha Mbolea"

Wakati huo huo, Serikali imeendelea kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kupitia kampeni ya "Mali Shambani, Silaha Mbolea" inayolenga kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.

Kupitia kampeni hiyo, wakulima wanahimizwa kutumia mbolea kulingana na mahitaji ya udongo na mazao wanayolima badala ya kutegemea aina moja ya mbolea kwa kila eneo.

Serikali pia imehimiza matumizi ya mbolea mbadala zinazozalishwa nchini, ikiwemo CAN, SA, Minjingu Top Dressing, Hakika NPK, Panda Power, Fomi Otesha, Yara Otesha na aina nyingine zinazozalishwa na viwanda vya ndani.

Wataalamu wa kilimo wanaeleza kuwa, matumizi ya mbolea mbadala yanaweza kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji huku yakiongeza ufanisi wa matumizi ya virutubisho kwenye udongo.

Katika maandalizi ya msimu mpya wa kilimo, Serikali imewataka wakulima kuhakikisha wanajiandikisha na kuhuisha taarifa zao katika mfumo wa ruzuku ili waweze kunufaika na programu za msaada wa pembejeo.

Pia,wamehimizwa kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo kuhusu matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza mavuno na kuboresha afya ya udongo.

Taswira ya msimu ujao

Kwa ujumla, hali ya upatikanaji wa mbolea nchini inaonesha kuwa Tanzania imeingia katika maandalizi ya msimu wa 2026/2027 ikiwa na akiba ya kutosha, mipango ya kuongeza shehena mpya na mfumo wa ruzuku unaoendelea kuwasaidia wakulima.

Ikiwa mwenendo wa kushuka kwa bei za mbolea duniani utaendelea, kuna matumaini ya kupungua kwa gharama za uzalishaji kwa wakulima na kuongeza uwezo wa sekta ya kilimo kuchangia ukuaji wa uchumi, usalama wa chakula na maendeleo ya taifa.

Kwa sasa, ujumbe wa Serikali kwa wakulima ni mmoja; mbolea ipo ya kutosha, maandalizi ya msimu mpya yanaendelea vizuri, na hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu upatikanaji wa pembejeo muhimu za kilimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here