DAR-Tanzania na Singapore zimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kwa kukubaliana kuongeza biashara na uwekezaji katika kilimo, bandari, uchumi wa kidijitali, maendeleo ya ujuzi, mazingira, afya na huduma za umma.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Ikulu, Dar es Salaam, wakati wa ziara ya kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam nchini, kwa mwaliko wa mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Rais Dkt.Samia amesema biashara kati ya nchi hizo imefikia dola za Marekani milioni 299, huku Singapore ikiwa na miradi 36 ya uwekezaji nchini Tanzania, kiwango ambacho bado hakiakisi fursa zilizopo.
“Uwezo wetu ni mkubwa zaidi ya kiwango cha biashara na uwekezaji tulichofikia sasa. Tumekubaliana kuongeza biashara na uwekezaji,” amesema Rais Samia. Viongozi hao wametaja viwanda, kilimo na usindikaji wa mazao, nishati, uchumi wa buluu na kijani, bandari, usafirishaji, utalii na teknolojia ya kidijitali kuwa maeneo ya kipaumbele na yenye nafasi kubwa ya ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore.
Halikadhalika, Rais Dkt. Samia ameialika Singapore kuwekeza teknolojia, utaalamu na mitaji katika uzalishaji mkubwa wa chakula nchini. Ushirikiano huo unalenga kuongeza uzalishaji na masoko ya mazao ya Tanzania, huku ukiisaidia Singapore kupanua vyanzo vyake vya chakula.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia pia ameeleza kuwa Tanzania, kama mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iko tayari kuanza mazungumzo ya mkataba wa biashara huria kati ya Jumuiya hiyo na Singapore.
Mkataba huo unatarajiwa kuongeza fursa za biashara na uwekezaji kati ya Singapore na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Rais Shanmugaratnam ameipongeza Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri kiuchumi barani Afrika, ikiwa na idadi kubwa ya vijana, rasilimali asilia na nafasi ya kimkakati katika Bahari ya Hindi.
“Tanzania imenipa taswira ya nchi inayojiamini katika uwezo wake na iliyo katika nafasi nzuri ya kutumia fursa zilizo mbele yake,” amesema Rais Shanmugaratnam.
Amesema, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaonesha dhamira ya Tanzania kuingia katika hatua mpya ya ukuaji. Pia alipongeza uongozi wa Rais Samia katika kufungua maeneo mapya ya ushirikiano na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la biashara kati ya Afrika Mashariki na Asia.
Viongozi hao pia walishuhudia kusainiwa kwa Mkataba wa Kutotoza Kodi Mara Mbili pamoja na hati za makubaliano kuhusu maendeleo ya ujuzi, masoko ya hewa ukaa, mashauriano ya nchi mbili na ushirikiano katika biashara.
Pande hizo pia zilikubaliana kushirikiana katika mageuzi ya kidijitali ya huduma za umma, mafunzo ya viongozi na watumishi, usimamizi wa mashirika ya umma, elimu ya ufundi, ubunifu na teknolojia.
Katika mazingira na mabadiliko ya tabianchi, Tanzania na Singapore zimejadili ushirikiano katika biashara ya kaboni, masoko ya kaboni, uhifadhi wa mazingira na nishati safi, Pamoja na shughuli za kiuchumi zinazolinda mazingira.
Ziara ya Rais Shanmugaratnam ni ya kwanza nchini kufanywa na Rais wa Singapore katika miaka 45 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Singapore.



