DAR-Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala aushukuru na kuupongeza uongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa namna wanavyoendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika masuala ya usimamizi wa maafa nchini.

Ametoa pongezi hizo leo Juni 9,2026 wakati wa kikao na uongozi wa WFP alipowatembelea katika Ofisi zao Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutoa shukran kwa namna wanavyotekeleza shughuli za usimamizi wa maafa kupitia program mbalimbali.
Brigedia Jenerali Ndagala aliongezea kuwa maeneo yanayotekelezwa ni pamoja na uboreshaji wa mifumo ya uratibu na teknolojia katika utoaji wa misaada ya kibinadamu wakati wa dharura, mipango ya mapema ya kujiandaa na dharura, utoaji wa kinga ya jamii wakati wa dharura, na upunguzaji wa vihatarishi vya maafa.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa WFP Tanzania, Bi.Christine Mendes, amesema ushirikiano huo umeimarishwa kupitia Miradi wanayoisimamia ambayo imeendelea kuwa na mchango katika kuimarisha uwezo wa kukabiliana na maafa nchini.









