DAR-Jamhuri ya Slovakia imeandika ukurasa mpya katika uhusiano wake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuzindua rasmi Ofisi ya Ubalozi wake jijini Dar es Salaam, hatua inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na maendeleo kati ya Tanzania na Sovakia.
Uzinduzi huo umefanywa kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Masuala ya Ulaya wa Slovakia, Mheshimiwa Juraj Blanár na Mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo Juni 11,2026 .
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Masuala ya Ulaya wa Jamhuri ya Slovakia, Mheshimiwa Juraj Blanár, amesema ufunguzi wa Ubalozi wa Slovakia ni hatua ya kimkakati inayodhihirisha umuhimu mkubwa ambao Serikali ya Slovakia inaipa Tanzania kama mshirika wake muhimu barani Afrika.
Amesema, Tanzania imeendelea kuwa kitovu muhimu cha diplomasia, biashara na maendeleo katika ukanda wa Afrika Mashariki, jambo linaloifanya kuwa lango la kuimarisha ushirikiano wa Slovakia na nchi za eneo hilo.
Amesisitiza kuwa,uwepo wa ubalozi huo utasaidia kuimarisha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya serikali hizo mbili na kuwezesha utekelezaji wa mipango ya pamoja katika nyanja mbalimbali za maendeleo na kuongeza kuwa “Slovakia inaona fursa kubwa ya kukuza ushirikiano na Tanzania katika sekta za biashara, uwekezaji, teknolojia, elimu, nishati, utalii na maendeleo ya rasilimali watu,” alisema.
Naye Mheshimiwa Blanár alikuwa nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia Juni 10 na 11,2026 ambapo alifanya mazungumzo na mwenyeji wake kwa lengo la kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kiuchumi ili kunufaisha uchumi wa mataifa hayo na wananchi wake.
Ameeleza kuwa ufunguzi wa ubalozi huo utafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa karibu zaidi kati ya sekta za umma na binafsi za nchi hizo mbili na kuweka mazingira bora ya kukuza biashara na uwekezaji kwa manufaa ya nchi zote.
Amepongeza juhudi za Tanzania katika kudumisha amani, utulivu na mazingira rafiki kwa uwekezaji, akieleza kuwa sifa hizo zimeifanya Tanzania kuwa mshirika wa kuaminika katika kufanikisha malengo ya pamoja ya maendeleo endelevu.
Ubalozi mpya wa Slovakia jijini Dar es Salaam unatarajiwa kuwa kiungo muhimu katika kurahisisha mawasiliano ya kidiplomasia, kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo na unaweka msingi imara wa kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu unaolenga ustawi wa wananchi wa Tanzania na Slovakia.
























