DAR-Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Slovakia zimethibitisha dhamira ya kuimarisha uhusiano ya kidiplomasia, ushirikiano wa kiuchumi, uwekezaji, pamoja na kubadilishana uzoefu wa kiutamaduni kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Hayo yamesemwa Juni 11,2026 wakati wa Jukwaa la Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Tanzania na Slovakia lililowakutanisha wawekezaji, viongozi wa biashara, wajasiriamali na wawakilishi wa serikali jijini Dar es Salaam.
Jukwaa hilo lilitoa fursa ya kujadili maeneo mapya ya ushirikiano na kukuza ukuaji wa uchumi endelevu na kubadilishana mawazo kuhusu namna ya kuongeza biashara, uwekezaji na ushirikiano katika sekta mbalimbali muhimu kwa maendeleo ya nchi hizo mbili.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alisema jukwaa hilo ni fursa ya kipekee ya kujenga ushirikiano imara na wa kudumu kati ya Tanzania na Slovakia.
Balozi Kombo alisisitiza kuwa katika dunia ya sasa balozi hazitumiki kama alama ya uhusiano wa kidiplomasia bali pia kama nyenzo muhimu za diplomasia ya uchumi, “msingi wa ushirikiano tayari umejengwa, sasa ni jukumu la wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa zilizopo kuongeza biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Slovakia."
Alibainisha Balozi Kombo na kueleleza kuwa mafanikio ya uhusiano huo yatapimwa kwa matokeo yatakayopatikana kutokana na mazungumzo na makubaliano ya wafanyabiashara na wawekezaji hao.
Balozi Kombo alinadi nafasi ya Tanzania kijiografia kama fursa kubwa siyo tu kwa soko la ndani, bali pia kwa soko la Kikanda la Afrika Mashariki (EAC) lenye nchi nane wanachama na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yenye nchi wanachama 16.
Alisema Tanzania na Slovakia, zinalengo la kuimarisha uhusiano wa kibiashara ambapo Tanzania husafirisha bidhaa za kilimo, madini ya thamani na bidhaa nyingine huku ikiagiza mashine na bidhaa za viwandani kutoka Slovakia, jambo linaloonyesha utegemeano na nguvu zinazotegemeana katika uchumi wa nchi hizo.
Naye, Waziri wa Mambo ya Nje na Masuala ya Ulaya wa Slovakia, Mhe. Juraj Blanár, alisema Slovakia inaiona Tanzania kama mshirika wa kimkakati na si soko pekee na kusisitiza utayari wao kuimarisha ushirikiano kupitia uhamishaji wa teknolojia, ubunifu, uwekezaji na kujenga uwezo wa rasilimali watu.Pia alieleza nia yao ya kuendeleza ushirikiano katika nyanja za elimu, utamaduni na uhusiano wa watu kwa watu.


























