Uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara zaidi licha ya changamoto za kiuchumi Kimataifa-BoT

DAR-Uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara licha ya changamoto za kiuchumi za kimataifa, ukikua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025 ikilinganishwa na asilimia 5.5 mwaka 2024.
Ukuaji huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na sekta za kilimo, madini, ujenzi na utalii, huku matarajio ya mwaka 2026 yakionesha ukuaji wa asilimia 6.3.

Aidha, mfumuko wa bei umeendelea kubaki ndani ya kiwango kinacholengwa cha asilimia 3 hadi 5, japokuwa umeanza kuongezeka kufuatia athari za migogoro inayoendelea Mashariki ya Kati.
Takwimu hizo zimewasilishwa na Dkt. Yamungu Kayandabila wakati akifungua rasmi Kikao cha 62 cha Kamati ya Maafisa wa Benki Kuu za nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kinachofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 9 hadi 10 Juni,2026.

Akizungumza kwa niaba ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt.Kayandabila alisema kuwa kikao hicho kinafanyika katika kipindi muhimu ambapo uchumi wa ukanda huo unakabiliwa na misukosuko mbalimbali, ikiwemo athari za mishtuko ya kiuchumi iliyotokea katika miaka sita iliyopita pamoja na changamoto zinazoendelea katika uchumi wa dunia.
Alisisitiza kuwa,katika mazingira hayo, kuna umuhimu mkubwa wa nchi wanachama kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuendeleza juhudi za ujumuishaji wa kiuchumi ili kuongeza uthabiti wa uchumi na uwezo wa kukabiliana na mishtuko.

Dkt.Kayandabila aliwataka wajumbe kutumia kikao hicho kama jukwaa la kujadili masuala ya kiufundi kwa kina na kutoa mapendekezo yatakayosaidia Magavana wa Benki Kuu kufanya maamuzi sahihi yanayoakisi hali halisi ya uchumi wa nchi wanachama.
Kikao hicho kinatarajiwa kujadili kwa kina masuala mbalimbali ya kifedha na kiuchumi kwa lengo la kuimarisha maendeleo na uthabiti wa uchumi katika ukanda wa SADC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here