Ujerumani yaunga mkono mradi wa uboreshaji huduma za usambazaji maji na usafi wa mazingira Songwe

DODOMA-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini mkataba wa msaada wa Euro milioni 20 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 60.7 kutoka Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kwa ajili ya kufadhili mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira katika miji ya Tunduma na Vwawa-Mlowo mkoani Songwe.Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba kwa upande wa Serikali ya Tanzania na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) nchini Tanzania, Bi. Vanessa Eidt.

‎Akizungumza baada ya utiaji saini wa mkataba huo, Dkt. Mwamba amesema kuwa,mradi unalenga kuchangia katika uboreshaji endelevu wa upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira, pamoja na usimamizi wa rasilimali za maji kwa watu wanaoishi katika miji ya Tunduma na Vwawa-Mlowo.
"Mradi huu utachangia katika kuongeza upatikanaji wa maji salama na safi ya kunywa na huduma endelevu za usafi wa mazingira kwa kujenga miundombinu ya usambazaji maji, kuunganisha wateja, Mtambo wa kutibu majitaka, ununuzi wa magari ya majitaka (exhauster), na ujenzi wa miundombinu ya usafi kwenye taasisi za umma kama vile ujenzi wa vyoo katika shule zilizochaguliwa," ameongeza Dkt. Mwamba.
Aidha, Dkt.Mwamba ameishukuru Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kwa msaada huo muhimu na kubainisha kuwa nchi hiyo imekuwa ikitoa misaada kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Dkt. Mwamba amebainisha kuwa, misaada hiyo imekuwa ikitolewa kwenye sekta za Maji, Afya, Uhifadhi wa Maliasili na Mazingira, Usimamizi wa Fedha za umma na Usawa wa Kijinsia ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi na ya kijamii nchini Tanzania.
Amesema,miradi hiyo inaendana na Dira ya Taifa ya mwaka 2025 inayoishia mwisho wa mwezi Juni 2026 na pia inaendana na Dira mpya ya 2050 na Mpango wa Taifa wa tatu wa Maendeleo wa Miaka mitano wa kuanzia mwaka 2020/21-2025/26 ambao unaishia June 2026 na pia inaendana na mpango mpya wa Nne wa Miaka Mitano wa mwaka 2026/27-2030/31.

Amesema,Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ipo tayari kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kwa maendeleo ya watu wake.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amesema,mradi huo umekuja katika wakati muhimu ambapo mabadiliko ya tabianchi pamoja na ukuaji wa haraka wa miji vinaongeza shinikizo katika rasilimali za maji.
Amesema,utekelezaji wa mradi huo utaimarisha usimamizi wa rasilimali za maji unaozingatia mabadiliko ya tabianchi na kuboresha upatikanaji wa huduma za maji kwa uhakika, hivyo kuchangia ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu ya kiuchumi katika maeneo husika.

Mhandisi Waziri amesema kuwa,Wizara ya Maji itaendelea kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu unafanyika kwa ufanisi, uwazi na kwa wakati, kwa kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha manufaa yake yanawafikia wananchi wa Tanzania.

Kwa upande wao, Naibu Balozi wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani nchini Tanzania, Bw. Manuel Muller na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) nchini Tanzania, Bi. Vanessa Eidt wamesema kuwa, Ujerumani ni mmoja wa washirika wakubwa wa maendeleo wa Tanzania, ikiwa na miradi ya zaidi ya euro milioni 400 inayotekelezwa kupitia misaada na ushirikiano wa kifedha huku Sekta ya maji ndiyo inayoongoza kwa kiwango cha uwekezaji, ikifuatiwa na sekta ya uhifadhi wa bayoanuwai, jambo linalodhihirisha umuhimu wa ushirikiano huu katika kuimarisha maendeleo endelevu nchini.

Wamesema wanaamani kuwa,wataendelea kufanya kazi pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kufikia malengo pamoja ya maendeleo jumuishi na endelevu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here