Uwanja wa Yanga SC eneo la Jangwani kugeuka shubiri,Mwinjilisti Temba aibua mapya

NA DIRAMAKINI

MHUBIRI na Mwinjilisti wa Kimataifa,Dkt. Alphonce Temba maarufu kama Fire Man, ameionya na kuitaka Klabu ya Yanga kuufikiria upya mpango wake wa kujenga uwanja mpya katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Amedai kuwa,mradi huo unaweza kuongeza msongamano wa magari na watu katika jiji ambalo tayari linakabiliwa na changamoto za miundombinu kutokana na ongezeko la idadi ya wakazi.

Akizungumza leo Juni 1,2026 jijini Dar es Salaam,Dkt.Temba amesema kuwa,badala ya kujenga uwanja huo katikati ya jiji, klabu hiyo inapaswa kutafuta eneo nje ya Dar es Salaam au pembezoni mwa jiji ili kuendana na mipango ya kisasa ya maendeleo ya miji mikubwa duniani.

Kwa mujibu wa Temba, Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuboresha na kupanua miundombinu ya barabara ili kupunguza msongamano wa magari, hivyo ujenzi wa miundombinu mikubwa ya michezo katikati ya jiji unaweza kwenda kinyume na juhudi hizo.

Amenukuu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, hususan Ibara ya 27(2) na 28, akisema kuwa wananchi wana wajibu wa kulinda rasilimali za taifa na kushiriki katika maendeleo ya nchi.

Hata hivyo, amesema hatakusudia kuchukua hatua za kisheria kupinga mradi huo licha ya kudai kuwa ana ushahidi na ushauri wa wataalamu wa sheria.

“Sitafungua kesi mahakamani. Badala yake nitamuomba Mungu kuzuia ujenzi huo kama hautazingatia maslahi mapana ya taifa na ustawi wa jiji,”amesema Dkt.Temba.

Katika maelezo yake, Temba amerejea matukio mbalimbali ambayo anaamini yalidhihirisha ushawishi wa maombi yake katika masuala ya kisiasa na kijamii ndani na nje ya Tanzania.

Ametaja utabiri wake wa mwaka 2004 kuhusu ushindi wa Jakaya Mrisho Kikwete ndani ya CCM na baadaye katika uchaguzi mkuu, pamoja na matukio mbalimbali aliyoyahusisha na siasa za Zambia na Malawi.

Aidha,amekumbusha tukio la mwaka 2025 alipotoa wito wa maombi dhidi ya maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika nchini, akidai kuwa matokeo ya siku hiyo yaliwafanya baadhi ya watu kuamini kuwa maombi hayo yalikuwa na mchango katika yale yaliyojitokeza.

Sasa, amesema amehamishia hoja yake kwenye mpango wa Yanga wa kujenga uwanja mpya, akisisitiza kuwa viongozi wa klabu hiyo wanapaswa kufanya tathmini ya kina kuhusu athari za muda mrefu za mradi huo kwa maendeleo ya jiji.

Temba amedai kuwa,baadhi ya nchi za Afrika zimekumbwa na changamoto za upangaji wa miji kutokana na uwekezaji mkubwa wa miundombinu katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu.

Ametaja Nigeria na Afrika Kusini kama mifano ya nchi ambazo, kwa mtazamo wake, zimewahi kukabiliwa na changamoto zinazofanana.

Pia amerejea simulizi za viongozi wa kidini mbalimbali barani Afrika ambao, kwa mujibu wa maelezo yake, waliwahi kutumia ushawishi wa kiroho kushawishi maamuzi ya viongozi wa serikali au taasisi katika nyakati tofauti za historia.

Hata hivyo, hadi sasa Klabu ya Yanga haijatoa tamko rasmi kujibu kauli za Temba wala kueleza kwa kina sababu za kuchagua eneo lililotangazwa kwa ajili ya mradi huo wa ujenzi wa uwanja mpya.

Wachambuzi wa masuala ya maendeleo ya miji wanaeleza kuwa,miradi mikubwa ya michezo inaweza kuwa na manufaa ya kiuchumi na kijamii ikiwa itaandaliwa kwa kuzingatia mipango ya matumizi ya ardhi, usafiri wa umma na ukuaji wa miji.

Aidha,wanasema tathmini za kitaalamu huwa muhimu kabla ya utekelezaji wa miradi mikubwa ili kuhakikisha inachangia maendeleo endelevu bila kuongeza changamoto za miundombinu.

Vilevile, kauli za Temba zimeungwa mkono na baadhi ya wananchi wakisisitiza kuwa,maamuzi kuhusu miradi mikubwa yanapaswa kuongozwa na tafiti za kitaalamu, sheria na mipango ya maendeleo ya taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here