WIPO yazindua Mradi wa Teknolojia kwa Maendeleo ya Jamii nchini Tanzania

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) wamezindua rasmi Mradi wa Teknolojia kwa Maendeleo ya Jamii nchini Tanzania.
Uzinduzi huo umefanyika leo Juni 1,2026 kupitia warsha ya kitaifa iliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo eneo la majaribio litakuwa Nyanda za Juu Kusini hususani Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, mwakilishi wa Afisa Mtendaji wa BRELA, ambaye ni Mkurugenzi wa Umiliki Ubunifu kutoka wakala huo, Loy Muhando amesema, katika mradi huo BRELA ndiyo ofisi ya umiliki ubunifu kwa upande wa Tanzania Bara.

Amesema, moja ya majukumu yake ni kutoa ulinzi wa bunifu mbalimbali, ambapo BRELA kutokana na jukumu lake hilo la kulinda miliki ubunifu kwa hapa nchini inafanya kazi kwa karibu sana na Shirika la Umiliki Bunifu Duniani (WIPO).

“Kufuatia ushirikiano huu, WIPO walikubali kutusaidia kutafuta teknolojia ambayo ni sahihi kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya jamii.
"Kwa hiyo, BRELA kama ofisi kiungo wa masuala ya umiliki ubunifu kwa upande wa Tanzania Bara ilifanya mawasiliano na WIPO Duniani na tukaona umuhimu wa kwenda mbali zaidi kwa sababu umiliki ubunifu zinalindwa, lakini kuona ni namna gani ambavyo tunatumia umiliki ubunifu kwa maendeleo ya jamii ndipo tukakubaliana sasa tuangalie bunifu mbalimbali ambazo ni sahihi, zilizopo kwenye kanzi data ambazo WIPO wanazo ili ziweze kutumika kwa ajili ya maendeleo ya jamii zetu hapa Tanzania.”

Amesema, hayo ndiyo matokeo ya mradi ambao umezinduliwa leo jijini Dar es Salaam huku matarajio yakiwa ni kufanyika kwa miezi 12.

Amesema, baada ya hapo mradi huo utaenda kwenye jamii nyingi zaidi kutoka mikoa ya Nyada za Juu Kusini ikijumuisha Njombe, Mbeya na Iringa kwa ajili ya kuwanufaisha wakulima na wafugaji.
Amesema, dhamira ni kupata vyakula vya uhakika kwa ajili ya mifugo huku mradi pia ukilenga kutafuta teknolojia ambayo itatumia mabaki ya chakula.

Amesema, kupitia mradi huo jamii nyingi zitanufaika ikiwemo wakulima,wafugaji na kupunguza mzigo wa kuagiza vyakula vya mifugo kutoka nje ya nchi.

“Kwa hiyo,mwisho wa siku tutakuwa tumeokoa kutumia fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza vyakula vya mifugo kutoka nje ya nchi.”

Pia, amesema kuna manufaa mengi ya kulinda bunifu ikiwemo kumpa haki mbunifu kwa kumtambua kuwa yeye ndiye wa haki husika.

Muhando amesisitiza kuwa, ubunifu usipolindwa unauweka katika hatari ya kuibiwa na mbunifu anapoteza.
Amesema,mbunifu anapolinda ubunifu anaupa thamani na mtu mwingine akitaka kuutumia mbunifu aliyeulinda anaweza kupata nafasi ya kutoa leseni ya matumizi au kuuza huo ubunifu wake.

“Kwa hiyo, ubunifu ukilindwa unakuwa njia ya kumuingizia kipato mbunifu kwa maana ya kutoa leseni ya matumizi, lakini pia unaweza ukahamishwa kwa mtu mwingine.Kinyume na hapo ni kwamba ubunifu usipolindwa mbunifu anakuwa hapati faida ya ubunifu wake.”

Amesema, sababu ni kwamba mtu yeyote anaweza kuutumia bila kumtambua mbunifu husika.

“Kwa hiyo, ni muhimu sana kulinda bunifu, lakini nchi yetu ina mifumo ya ulinzi wa miliki ubunifu, na mifumo hii pia inakwenda mbali zaidi mpaka tumeunganishwa na mifumo ya kikanda ya umiliki ubunifu, lakini pia Kimataifa tunaona hata ushirikiano wetu huu hapa na WIPO."
Amesema, bunifu zinapokuwa zimelindwa zinakuwa na taarifa ambazo ni muhimu zaidi kwa ajili ya maendeleo ya teknolojia.

Pia, amesema bunifu hizo hususani upande wa ataza zinapokuwa zimeisha muda wake, mtu mwingine anaweza kutumia teknolojia zilizopo kwenye bunifu hizo ili kuweza kuleta maendeleo mbalimbali katika jamii na Taifa kwa ujumla.

“Ndiyo maana katika mradi huu tutatumia teknolojia ambayo bunifu zake zilikwisha lindwa, lakini zikapita muda wake na sisi tumeona ni teknolojia sahihi kwa ajili ya kuleta maendeleo katika nchi yetu.”

WIPO

Purevdorj Vaanchig ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Kuratibu Nchi Zinazoendelea Sana (LDCs), Nchi Zinazoendelea Zisizo na Bandari (LLDCs) na Mataifa Yanayoendelea ya Visiwa Vidogo (SIDS) ndani ya Shirika la WIPO ameeleza kuwa,mradi huo unalenga kuimarisha uwezo wa jamii kunufaika na teknolojia zinazotokana na tafiti na ubunifu wa ndani kupitia teknolojia zilizopita.
Amesema, mradi huo una manufaa mengi ikiwemo kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani kuhusu namna ya kutumia teknolojia na namna ya kutekeleza mradi huo kwa jamii ya Watanzania.

Pia,amesisitiza umuhimu wa mifumo madhubuti ya haki miliki katika kulinda na kuendeleza ubunifu unaoweza kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii.

Mradi huo unakusudia kuibua na kuendeleza teknolojia zinazotoa suluhisho kwa changamoto za maendeleo katika sekta ya kilimo na mifugo kwa sasa.

Kupitia mradi huu, wataalamu wa WIPO na Watanzania watafanya utafiti kwenye kanzidata za hataza duniani kubaini teknolojia ambazo ziko wazi kutumika,zimeisha muda wa ulinzi au hazijalindwa Tanzania.

Aidha,NM-AIST itazirekebisha kwa kutumia malighafi za hapa nchini, huku BRELA ikisaidia usajili wa biashara kwa vikundi vitakavyotumia teknolojia hizo.

Aidha, utawezesha uhamishaji wa teknolojia na maarifa kutoka taasisi za utafiti kwenda kwa watumiaji wa mwisho katika jamii ili kuongeza tija na kuboresha maisha ya wananchi.

COSTECH

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),Dkt.Amos Nungu amesema, miongoni mwa vipaumbele ni kuangazia umiliki bunifu, kuangalia namna ya kutumia taarifa zilizopo ili kuangalia ni zipi ambazo zinafaa kwa jamii iliyopo kwa sasa.
Amesema,watakwenda kwenye kanzi data ya WIPO duniani kuangalia teknolojia sahihi kwa ajili ya mazingira yetu ambazo tayari zimeshamaliza muda wake kulingana na ulinzi ili waweze kuzitumia nchini.

"Tumechagua eneo la kilimo biashara na ufugaji, kikubwa zadi tunaangalia kwamba tuna mashine nyingi za kuzalisha chakula cha mifugo mfano.

"Lakini, hizi mashine nyingi tunazisapoti hapa COSTECH kupitia MAKISATU (Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu), lakini tukitaka kwenda kwenye hatua inayofuata kwa ajili ya uzalishaji mkubwa inakuwa shida kwa wawekezaji wakubwa kwa sababu zile mashine zinakuwa hazina michoro fulani ambayo inaweza kutambulika.

"Sasa akija mwekezaji akataka kwenda kwenye mchakato wa uzalishaji viwandani inakuwa changamoto, kwa hiyo ushirikiano tunaoufanya sasa hivi tumechagua taasisi moja ambayo tutashirikiana nayo ili kwenda kwenye hizo kanzi data kutafuta teknolojia sahihi."

Amesema, wakishafanikisha Taasisi ya Nelson Mandela watatumia taarifa hizo kutengeneza sampuli kifani,baada ya hapo wataangalia kwa pamoja kuwa na business model ili kuona namna ambavyo wataweza kutumia sampuli hiyo katika jamii.

Amesema, wamechangua Njombe kama eneo la majaribio na baada ya hapo watakaa chini ili kuandika andiko kwa ajili ya kushirikiana na wadau ili kufanya uzalishaji mkubwa.

Aidha, amesema baada ya uzinduzi huu wa leo yatafanyika mafunzo ya siku tano ambayo yatawaleta pamoja wataalamu mbalimbali ili baada ya hapo kupata picha kamili na waweze kutembea pamoja.
Amesema, baada ya hatua hiyo kukamilika watakuwa wanawasaidia vijana wa Tanzania kupata haki miliki ikiwemo kuwa na bunifu na sampuli ambazo zinaweza kwenda sokokoni.

Pia, amesema mradi huo ukikamilika licha ya kuwa kivutio kwa wawekezaji vilevile utakuwa na faida nyingi kwa jamii,vijana na Taifa kwa ujumla.

Miongoni mwa faida hizo ni pamoja na kupata sampuli ambayo ina uthibitisho duniani licha ya kwamba hiyo teknolojia inaweza kuwa imetumika mfano Marekani,Ulaya na pengine lakini wataichukua na kuja kuitumia hapa Tanzania.

Jambo la pili, teknolojia hiyo wanaiweka katika mazingira ya Tanzania kwani Taasisi ya Nelson Mandela ipo katika mchakato huo kwa kuwa, ni taasisi ya teknolojia ambayo itashiriki katika utekelezaji huo.
Faida ya tatu, amesema watashirikiana na wadau wengine ili kuona wanapotaka kwenda sokoni kupitia taarifa hizo watafanyaje na kila hatua watashirikiana na WIPO.

Amesema, kupitia mradi huo wa mfano wataunda kamati ya utekelezaji ambayo watashirikiana hatua kwa hatua na baada ya kukamilika watajifunza ili baada ya eneo la mfano Njombe iweze kupelekwa nchi nzima.

Aidha, licha ya Nelson Mandela watashirikiana na vyuo vingine huku jukumu kubwa la COSTECH likiwa ni kuratibu programu yote.

Amesema, sampuli kifani ikishapatikana moja inakuwa ni business model ambapo wakiitengeneza Nelson Mandela wataenda kuijaribu kule Wanging’ombe na ikishathibitisha sasa uzalishaji mwingi unaanza kwa ajili ya nchi nzima.

Taasisi ya Nelson Mandela

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Taasisi ya Nelson Mandela, Profesa Thomas Kivevele ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu katika taasisi hiyo amesema, wao ni miongoni wa wadau katika mradi huo ambapo kwa asilimia kubwa watakuwa kwenye eneo la utafiti na ubunifu.
Amesema, watakuwa wanachakata data ambazo zinatoka kwenye chanzo huko Njombe na kuja na ubunifu kwa ajili ya kutatua changamoto ya chakula cha mifugo mkoani humo.

Amesema, mchakato hadi kuja na sampuli kifani utakuwa wa mwaka mmoja na wataelekea kwenye uzalishaji mkubwa.

Amesema, kikubwa ni kuangalia namna ambavyo watatumia hizo data ambazo watazipata huko Njombe ili kuja na sampuli kifani ambayo wanaamini itafanya kazi vizuri ili kuelekea hatua nyingine ya uzalishaji mkubwa.

Amesema, lengo la mradi huo ni kukuza uwezo wa watanzania kwani Nelson Mandela itakuwa ni sehemu ya wataalamu ikiwa na wataalamu wabobezi katika hilo eneo.

Amesema, kutokana na wataalamu waliopo Nelson Mandela wataweza kusambaza hayo maarifa hata kwa watu ambao wapo vijijini ambao wanaweza kukuza huo uwezo wa Watanzania wengi kuweza kujua hilo eneo na kuja teknolojia nyingi zaidi ambazo zinaweza zikasaidia katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja,jamii na Taifa kwa ujumla.

Mnufaika

Miongoni mwa wanufaika wa mradi huo utakapotelekezwa, Annaupendo Edward ambaye ni mkulima na mfugaji kutoka Mkoa wa Njombe amesema kuwa, mradi huo unatarajiwa kuanza wilayani Wanging’ombe kwa majaribio.
Amesema, mategemeo yake kama mkulima na mfugaji endapo wataalamu hao na wawekezaji watafanikiwa kutengeneza mashine za ubunifu ambazo zitasaidia kutengeneza vyakula vya mifugo na mabaki ya chakula kutengeneza mbolea itawasaidia wao kama wakulima kupata uhakika wa chakula cha mifugo kwa wakati.

Pia, amesema itasaidia kuongeza thamani kwa wafugaji na wakulima kwani kwa sasa wana changamoto kubwa ya kupata chakula cha mifugo na mbolea.

“Kwa hiyo, mradi huu kama utakamilika utakuwa ni chachu kubwa na utaongeza tija kubwa kwa wakulima na wafugaji na utarahisisha pia wafugaji kupunguza gharama kubwa katika ufugaji kwani upatikanaji wa chakula ni mgumu.”
Amesema, katika wilaya yao kuna changamoto ya upatikanaji wa chakula cha mifugo na mbelea, hivyo wanatarajia ujio wa teknolojia mpya utawawezesha kupata urahisi wa uzalishaji mali.

Uzinduzi wa mradi huo unaonekana kuwa hatua muhimu katika juhudi za Tanzania za kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo za kufikia maendeleo jumuishi na endelevu, sambamba na utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here