DAR-Serikali ya Tanzania imeendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa mafanikio makubwa baada ya kuvutia wawekezaji kutoka Urusi katika sekta mbalimbali za kimkakati, hatua inayotarajiwa kuongeza ukuaji wa uchumi, ajira na maendeleo ya viwanda nchini. Mafanikio hayo yamepatikana kufuatia ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi iliyofanyika kuanzia Juni 3 hadi 6, 2026.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari uliolenga kueleza mafanikio ya ziara hiyo, Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga, amesema Tanzania imepokea mwitikio mkubwa kutoka kwa wawekezaji wa Urusi walioonesha nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali muhimu za maendeleo ya taifa.Balozi Ulanga amesema,wawekezaji hao wamevutiwa na fursa zilizopo nchini katika sekta za madini ya kimkakati, nishati, afya na dawa, kilimo pamoja na teknolojia ya kidijitali. Ameeleza kuwa maeneo hayo yanachukuliwa kuwa nguzo muhimu za maendeleo ya uchumi wa Tanzania kutokana na mchango wake katika kuongeza uzalishaji, ajira na mapato ya taifa.
Kuhusu sekta ya madini, amesema kampuni za Urusi zimeonesha dhamira ya kushiriki katika miradi ya uchimbaji na maendeleo ya madini muhimu kama uranium, nickel na graphite. Alibainisha kuwa tayari kuna kampuni ya Urusi inayoshiriki katika mradi wa uranium nchini, jambo linalodhihirisha kuimarika kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi katika sekta ya madini.
Aidha, amesema kampuni kubwa za Urusi zimeonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya nishati hususan mafuta na gesi asilia, huku kampuni ya Gazprom ikitajwa kuwa miongoni mwa kampuni zilizoonesha utayari wa kushiriki katika shughuli za utafutaji na maendeleo ya rasilimali hizo nchini.
Vilevile, kampuni za Urusi zimeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika uzalishaji wa dawa na chanjo ili kuimarisha uwezo wa ndani wa uzalishaji wa bidhaa za afya na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
Kwa upande wa kilimo na uchumi wa kidijitali, Balozi Ulanga amesema wawekezaji wa Urusi wanatarajiwa kushirikiana na Tanzania katika matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo, usindikaji wa mazao na upanuzi wa masoko ya bidhaa kama korosho, kahawa na chai.Pia, kampuni za teknolojia na startup kutoka Urusi zinatarajiwa kusaidia kukuza ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa nchini. Amesisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za Serikali kutumia diplomasia ya uchumi kuvutia mitaji, teknolojia na utaalamu wa kimataifa kwa manufaa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania.











