Vigogo saba wa Umeme nchini Uganda wafutwa kazi

NA DIRAMAKINI

KAMPUNI ya Usambazaji Umeme nchini Uganda (UEDCL) imefuta mikataba ya ajira ya maofisa wake saba waandamizi, hatua inayozidi kuonesha mabadiliko makubwa yanayoendelea ndani ya taasisi hiyo tangu ilipochukua rasmi usimamizi wa mtandao wa usambazaji umeme kutoka kampuni ya Umeme mwezi Aprili,mwaka 2025.
Maofisa hao walikuwa miongoni mwa viongozi waandamizi waliolazimishwa kuondoka kazini kwa muda mwezi Februari,mwaka huu wakati Wizara ya Nishati ya Uganda ilipomsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa UEDCL, Paul Mwesigwa, na wakati huo huo kumuondoa madarakani Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Lydia Ochieng-Obbo.

Hatua ya kufutwa kwa mikataba yao imekuja kufuatia wiki kadhaa za uchunguzi wa ndani uliolenga kutathmini utendaji kazi, mazingira ya kikazi na ufanisi wa taasisi hiyo katika kipindi cha mpito.

Maofisa waliokumbwa na hatua hiyo ni Mkuu wa Ukaguzi wa Ndani, Justine Nakagiri Ssemwanga; Mkuu wa Rasilimali Watu na Utawala, Boniface Barongo; Meneja wa Ushirikiano wa Rasilimali Watu, Beatrice Tumuheirwe; Mkuu wa Mawasiliano na Mahusiano na Wadau, Jonan Kiiza; Mkuu wa Huduma za Uhandisi na Ufundi, Protaze Tibyakinura; Mkuu wa Teknolojia na Mifumo ya Kidijitali, Barbrah Kyomuhendo pamoja na Meneja wa Mifumo ya Maombi ya Teknolojia, Geoffrey Musafu.

Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani vinavyofahamu suala hilo, viongozi hao walijulishwa kuwa mikataba yao haitahuishwa upya baada ya Juni 30,mwaka huu, jambo linalomaanisha mwisho wa utumishi wao ndani ya shirika hilo.

Vyanzo kutoka Wizara ya Nishati vimethibitisha kuwepo kwa hatua hiyo ya kufutwa kwa mikataba, ingawa vilielekeza waandishi wa habari kuwasiliana moja kwa moja na UEDCL kwa maelezo zaidi.

"Mimi siwezi kuthibitisha rasmi, lakini ninachofahamu ni kwamba Kaimu Mkurugenzi Mtendaji amelifukuza kundi hilo. Kwa maelezo zaidi wasiliana na UEDCL kupitia msemaji wa muda, Stephen Ilungole," kilisema chanzo kimoja kutoka wizara hiyo.

Hata hivyo, juhudi za kupata maoni ya msemaji huyo hazikufanikiwa hadi wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hii.

Hatma ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Paul Mwesigwa, bado haijawekwa wazi. Tangu aliposimamishwa kazi kwa muda kufuatia malalamiko kuhusu utendaji wa shirika, ongezeko la malalamiko ya wateja pamoja na kupanda kwa kiwango cha upotevu wa umeme, hajarejea kazini wala kutolewa tamko rasmi kuhusu mustakabali wake.

Kusimamishwa kwake kulitafsiriwa na wachambuzi kama ishara ya shinikizo kubwa kutoka serikalini kwa UEDCL kuthibitisha uwezo wake wa kusimamia sekta ya usambazaji umeme baada ya kuondoka kwa Umeme, ambayo ilisimamia huduma hiyo kwa zaidi ya miaka 20 chini ya mfumo wa ubia wa sekta binafsi.

Tangu ilipochukua jukumu la kusimamia mtandao wa taifa wa usambazaji umeme, UEDCL imekuwa chini ya uchunguzi mkali wa umma kutokana na ongezeko la kukatika kwa umeme, kuchelewa kwa huduma za kuwaunganisha wateja wapya pamoja na kuongezeka kwa upotevu wa umeme katika mfumo wa usambazaji.

Taarifa zinaonesha kuwa,kiwango cha upotevu wa umeme kiliongezeka kutoka asilimia 15 hadi asilimia 19 wakati wa kipindi cha mpito, jambo lililozua wasiwasi mkubwa kuhusu uwezo wa shirika hilo kufikia malengo ya serikali katika sekta ya nishati.

Katika juhudi za kuimarisha utendaji kazi na kujaza nafasi zilizoachwa wazi, UEDCL imekuwa ikiteua viongozi wa muda katika idara mbalimbali muhimu, wengi wao wakiwa ni watumishi waliowahi kufanya kazi katika kampuni ya Umeme.

Miongoni mwa walioteuliwa kwa nafasi za muda ni Joselynne Rwakakooko anayehudumu kama Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Sylver Hategekimana anayesimamia Uhandisi, Isaac Katewanga upande wa Biashara, Samuel Omoding katika Rasilimali Watu, Stephen Ilungole katika Mawasiliano ya Taasisi, Nickson Ahabwe katika Ukaguzi wa Ndani, Richard Opiyo katika Teknolojia na Mifumo ya Kidijitali, Francis Ddamulira katika Usimamizi wa Mifumo ya Maombi na Christine Atuhaire katika Ushirikiano wa Rasilimali Watu.

Aidha,wachambuzi wa sekta ya nishati wanaona uteuzi huo kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha uwezo wa kiutendaji wa kampuni na kuoanisha mfumo wake wa uongozi na mwelekeo mpya wa kimkakati unaokusudiwa na serikali.

Mabadiliko hayo yanakuja wakati Uganda ikiwa imeweka malengo makubwa ya kupunguza upotevu wa umeme, kuongeza upatikanaji wa huduma za nishati kwa wananchi na kuboresha uhakika wa huduma nchini kote.

Hata hivyo, kufanikisha malengo hayo kutahitaji UEDCL kuonyesha uwezo wa kusimamia kwa ufanisi mtandao ambao kwa zaidi ya miongo miwili uliendeshwa na kampuni binafsi.

Mbali na changamoto za kiutendaji, shirika hilo pia linakabiliwa na matarajio makubwa kutoka kwa wananchi pamoja na uangalizi wa karibu wa viongozi wa kisiasa wanaotaka kuona maboresho ya haraka katika utoaji wa huduma.

Wakati huo huo, Serikali ya Uganda inaendelea na mchakato wa usuluhishi wa kisheria dhidi ya Umeme kuhusu malipo yenye utata ya dola za Marekani milioni 234.7 yaliyotokana na makubaliano ya ununuzi wa mali za kampuni hiyo, suala ambalo linaendelea kuvuta hisia za wadau wengi wa sekta ya umeme nchini humo.

Kwa sasa, changamoto kubwa kwa UEDCL siyo tu kufanya mabadiliko ya viongozi, bali ni kuthibitisha kwa wateja, wawekezaji na watunga sera kwamba mageuzi yanayoendelea yatazaa matokeo chanya katika utoaji wa huduma bora, kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kuimarisha sekta ya umeme ya Uganda kwa ujumla.

Iwapo mabadiliko haya makubwa ya uongozi yatafanikiwa kufikia malengo hayo, bado ni swali linalofuatiliwa kwa karibu na wadau wa sekta ya nishati nchini Uganda na katika ukanda wa Afrika Mashariki.(CEO East Africa Magazine)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here