DODOMA-Banda la Tume ya Madini limeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa mamia ya wananchi wanaotembelea Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, huku wengi wakijitokeza kupata elimu kuhusu sekta ya madini, huduma zinazotolewa na Tume pamoja na fursa zilizopo katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini.

Miongoni mwa waliotembelea banda hilo ni Lusajo Luena kutoka Dodoma, ambaye amesema elimu aliyoipata imemwezesha kuelewa taratibu za upatikanaji wa leseni za madini na wajibu wa wamiliki wa leseni katika kuendeleza maeneo yao ya uchimbaji.
"Kabla ya kufika hapa sikuwa na uelewa wa kina kuhusu namna leseni za madini zinavyotolewa na kusimamiwa. Leo nimepata elimu ya kutosha kuhusu taratibu mbalimbali na umuhimu wa kuzingatia sheria za madini," amesema Luena.
Kwa upande wake, Joyce Kitundu kutoka Dodoma amesema maelezo aliyopata katika banda hilo yamemsaidia kufahamu mchango mkubwa wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa taifa na namna Serikali inavyosimamia rasilimali za madini kwa manufaa ya wananchi."Nimejifunza kuwa sekta ya madini ni nguzo muhimu ya maendeleo ya nchi. Pia nimeelewa majukumu ya Tume ya Madini katika kusimamia shughuli za uchimbaji na biashara ya madini nchini,"amesema Kitundu.
Naye Glory Daudi kutoka Kondoa amesema elimu aliyopata imefungua fursa mpya za uelewa kuhusu ushiriki wa vijana na wanawake katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta ya madini."Nimefurahishwa na elimu niliyopewa kuhusu fursa zilizopo kwenye sekta ya madini. Sasa nimeelewa kuwa si lazima mtu awe mchimbaji pekee, kwani kuna fursa nyingi za biashara na utoaji huduma zinazozunguka sekta hii," amesema Daudi.
Tume ya Madini inaendelea kutumia maonesho hayo kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake, huduma mbalimbali zinazotolewa pamoja na kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.


