Watu 42 wafukuzwa Ireland na kurejeshwa Afrika Kusini kwa ndege maalumu

NA DIRAMAKINI

JUMLA ya raia 42 wa Afrika Kusini wameondolewa nchini Ireland na kurejeshwa katika nchi yao kupitia operesheni maalumu ya uhamishaji iliyosimamiwa na Kitengo cha Taifa cha Uhamiaji cha Polisi wa Ireland (Garda National Immigration Bureau-GNIB), kwa mujibu wa amri za kufukuzwa zilizotolewa na Waziri wa Sheria wa nchi hiyo, Jim O’Callaghan.
Operesheni hiyo ilitekelezwa siku ya Alhamisi ambapo wahusika wote waliondolewa rasmi kutoka Ireland kwa mujibu wa sheria za uhamiaji za nchi hiyo.

Waliosafirishwa walikuwa raia wa Afrika Kusini waliokuwa wamepewa amri za kuondoka nchini humo baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka husika, kundi hilo lilijumuisha watu wazima 27, kati yao wanaume tisa na wanawake 18, pamoja na watoto na vijana 15 ambao walikuwa sehemu ya familia mbalimbali zilizohusika katika zoezi hilo.

Wahamiaji hao waliondolewa kwa kutumia ndege maalumu iliyokodiwa na serikali, ambayo iliondoka jijini Dublin mchana wa Alhamisi na kuwasili nchini Afrika Kusini asubuhi ya Ijumaa.

Mamlaka za Ireland zimeeleza kuwa,miongoni mwa watu waliofukuzwa walikuwepo watu wawili waliokuwa wamepatikana na hatia ya makosa ya jinai ndani ya Ireland.

Kufukuzwa kwao kunatajwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha utekelezaji wa sheria za uhamiaji na kudumisha usalama wa umma nchini humo.

Akizungumza kuhusu operesheni hiyo, msemaji wa Jeshi la Polisi la Ireland amesema,hatua hiyo inaunga mkono shughuli zinazoendelea za vyombo vya usalama nchini kote katika kusimamia na kutekeleza sheria za uhamiaji.

“Maafisa wa Garda wanaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Sheria katika utekelezaji wa sera za uhamiaji, pamoja na Huduma ya Magereza ya Ireland katika kusimamia operesheni kama hizi,"amesema msemaji huyo.

Hatua hiyo inakuja wakati Ireland ikiendelea kuimarisha mifumo yake ya usimamizi wa wahamiaji.

Mwaka 2024, Wizara ya Sheria ilichukua rasmi majukumu ya usajili wa kiutawala wa wahamiaji yaliyokuwa yakitekelezwa awali na Jeshi la Polisi la Garda, hatua iliyolenga kuongeza ufanisi katika usimamizi wa masuala ya uhamiaji nchini humo.

Operesheni ya kuwarejesha raia hao wa Afrika Kusini inaonesha msimamo wa serikali ya Ireland katika kuhakikisha sheria za uhamiaji zinafuatwa kikamilifu, huku mamlaka zikisisitiza kuwa hatua zote zinazochukuliwa hufanyika kwa kuzingatia taratibu za kisheria na haki za binadamu. (NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here