DAR-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Masuala ya Ulaya wa Slovakia, Mhe. Juraj Blanár, ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi kuanzia tarehe 10 hadi 11 Juni 2026. Ziara hiyo inalenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa maendeleo kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Slovakia.
Baada ya mazungumzo yao ya faragha, viongozi hao waliongoza kikao cha uwili kilichojadili masuala mbalimbali yenye maslahi ya pamoja, ikiwemo kuimarisha ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji, kilimo, mageuzi ya kidigitali na usalama wa mitandao, utalii, nishati mbadala, elimu na afya.
Pande zote mbili zimeridhishwa na mwenendo mzuri wa mahusiano kati ya nchi hizo na kuahidi kuendelea kushirikiana katika maeneo yenye manufaa kwa wananchi wa mataifa hayo mawili.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Waziri Kombo amemshukuru Mhe. Blanár kwa kutembelea nchini na kuipongeza Slovakia kwa hatua ya kufungua Ubalozi wake nchini Tanzania, hatua ambayo imeongeza fursa za ushirikiano wa karibu zaidi katika nyanja mbalimbali za maendeleo na biashara.
Kadhalika Mhe. Waziri Kombo alitumia fursa hiyo kuikaribisha Jamhuri ya Slovakia kushiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai, 2026 ambapo wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi hiyo wanakaribishwa kuja kujionea fursa mbalimbali zilizopo nchini.
Kwa upande wake, Mhe. Waziri Blanár ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano unaoendelea kutolewa na kusisitiza dhamira ya Slovakia ya kuendelea kuimarisha mahusiano ya kirafiki na ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania.
Aliongeza kusema nchi yake ina nia ya dhati ya kushirikiana na Tanzania katika maeneo yote yaliyoainishwa wakati wa mazungumzo yao na kwamba katika kuipa uzito ziara yake hapa nchini, ameambatana na wafanyabiashara wapatao 35 ambao wana nia ya kuangalia fursa zilizopo kwa ajili ya kuja kuwekeza.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuendeleza ushirikiano wa pande mbili na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi kati ya Tanzania na Slovakia.
Mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam yalihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa, Balozi wa Tanzania nchini Slovakia mwenye makazi nchini Austria, Mhe. Naimu Aziz, Balozi wa Slovakia nchini, Mhe. Ivan Lancaric, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Balozi Mindi Kasiga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bi. Ellen Maduhu na Viongozi wengine kutoka Tanzania na Slovakia.


























