NA DIRAMAKINI
WAZIRI Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer ametangaza kujiuzulu wadhifa wake baada ya kukabiliwa na shinikizo kubwa la kisiasa kutoka ndani ya chama tawala cha Labour Party, kufuatia matokeo yasiyoridhisha ya uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na kuongezeka kwa migawanyiko ya kisiasa ndani ya chama hicho.
Akizungumza mbele ya makazi rasmi ya Waziri Mkuu ya 10 Downing Street mnamo Juni 22, 2026, Starmer amesema tayari amemuarifu King Charles III kuhusu uamuzi wake wa kuachia madaraka.
Aidha, amebainisha kuwa,ataendelea kuhudumu kama Waziri Mkuu wa mpito hadi pale chama chake kitakapomchagua mrithi atakayechukua nafasi hiyo.
Uamuzi huo unahitimisha kipindi cha takribani miaka miwili ya uongozi wa Starmer, ambaye aliingia madarakani mwezi Julai 2024 baada ya kuiongoza Labour kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa Uingereza.
Hata hivyo, katika miezi ya karibuni serikali yake ilikumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo shinikizo la hali ya uchumi, kupungua kwa imani ya wananchi kwa serikali, pamoja na ukosoaji mkali kutoka kwa wabunge wa chama chake.
Wachambuzi wa siasa nchini humo wanaeleza kuwa,matokeo mabaya ya uchaguzi wa mitaa yaliyokikosesha Chama cha Labour uungwaji mkono katika maeneo kadhaa muhimu yalichangia kwa kiasi kikubwa kuzorota kwa nafasi ya Starmer ndani ya chama.
Hali hiyo ilizidishwa na wito kutoka kwa baadhi ya viongozi na wabunge wa Labour waliotaka mabadiliko ya uongozi ili kukirejesha chama katika mkondo wa ushindani wa kisiasa.
Kujiuzulu kwa Starmer sasa kunafungua rasmi mbio za kuwania uongozi wa Labour, huku Andy Burnham akitajwa kuwa miongoni mwa viongozi wenye nafasi kubwa ya kurithi uongozi huo.
Burnham tayari ameonesha nia ya kuwania nafasi hiyo, huku akipata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya viongozi waandamizi ndani ya chama.
Kwa mujibu wa ratiba inayotarajiwa kutangazwa na viongozi wa Labour, mchakato wa kumpata kiongozi mpya utaanza mwezi Julai na kukamilika kabla ya Bunge la Uingereza kurejea kutoka mapumzikoni mwezi Septemba,mwaka huu.
Mrithi wa Starmer atachukua jukumu la kuiongoza serikali katika kipindi ambacho taifa hilo linaendelea kukabiliana na changamoto za kiuchumi, huduma za kijamii na mazingira mapya ya ushindani wa kisiasa nchini humo.
Kuondoka kwa Starmer kunatajwa kuwa tukio jingine muhimu katika historia ya siasa za Uingereza, likiongeza idadi ya viongozi waliolazimika kuondoka madarakani kabla ya kumaliza vipindi vyao kamili katika muongo uliopita.
Hatua hiyo inatarajiwa kuwa na athari kubwa kwa mwelekeo wa kisiasa wa Uingereza na mustakabali wa Chama cha Labour katika uchaguzi mkuu ujao.
