Waziri Ridhiwani Kikwete awauma sikio Maafisa Tawala na Rasilimali Watu nchini

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete leo Juni 1,2026 amefungua Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Tawala na Rasilimali Watu uliofanyika katika Ukumbi wa Jenerali Mabeyo jijini Dodoma, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia taratibu za utumishi pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Mkutano huo umejumuisha Maafisa Tawala na Rasilimali Watu kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali, taasisi zinazojitegemea pamoja na mamlaka za Serikali za Mitaa.

Pia,mkutano huo wa kila mwaka unatoa jukwaa kwa wataalamu hao kujadili masuala mbalimbali yanayohusu taaluma zao, kubadilishana uzoefu na kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazojitokeza katika usimamizi wa rasilimali watu na utawala wa umma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mhe.Kikwete amesema kuwa,mkutano huo una umuhimu mkubwa katika juhudi za Serikali za kuendelea kuboresha utendaji wa utumishi wa umma kwa kuwajengea uwezo wataalamu wanaosimamia rasilimali watu na masuala ya utawala katika taasisi za umma.
Ameeleza kuwa,Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeendelea kuandaa mikutano hiyo kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali Kuu na wataalamu waliopo katika taasisi mbalimbali za umma, jambo linalochangia kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Waziri huyo amewakumbusha washiriki wa mkutano huo umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Aidha, amewataka kuimarisha ushirikiano na mawasiliano kati ya ofisi zao na Ofisi ya Rais- Utumishi ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao ya kazi.
“Ni muhimu kuendelea kuimarisha mawasiliano kati ya taasisi zenu na Ofisi ya Rais-Utumishi ili changamoto mbalimbali ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa wakati. Vilevile, tunapaswa kuendelea kutumia kikamilifu mifumo ya kidijitali iliyobuniwa na Serikali kwa lengo la kuongeza ufanisi,uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi."

Mhe. Kikwete pia amesisitiza matumizi ya teknolojia za habari na mawasiliano, hususan mifumo mbalimbali iliyotengenezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, akieleza kuwa mifumo hiyo imekuwa nyenzo muhimu katika kuboresha usimamizi wa rasilimali watu na utoaji wa huduma serikalini.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alitumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo na uongozi wake ambao umeendelea kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa ufanisi na kuimarisha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Aidha, alitaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika sekta ya utumishi wa umma, ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa watumishi, upandishaji wa madaraja kwa watumishi wenye sifa stahiki.

Sambamba na ulipaji wa madeni yanayotokana na mishahara na likizo, hatua ambazo zimechangia kuongeza motisha na ustawi wa watumishi wa umma nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here