NA DIRAMAKINI
MTAALAMU wa Masuala ya Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Mtandao, Yusuph Kileo amemshukuru Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kutambua mchango wake unaoendelea katika kuimarisha usalama wa mtandao, uchunguzi wa kisayansi wa makosa ya mtandao (Digital Forensics) pamoja na juhudi za kulinda watumiaji wa mifumo ya kidijitali nchini Tanzania.
Mtaalamu wa Masuala ya Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Mtandao, Yusuph Kileo.

Ametoa shukurani hizo, baada ya Juni 19,2026 katika Usiku wa Tanzania ya Thamani uliofanyika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Majaliwa kumpongeza kwa kazi nzuri anayofanya ikiwemo kushauri na kutoa elimu kwa Watanzania kupitia njia mbalimbali kama vyombo vya habari.
Kileo amesema kuwa,utamaduni wa kutambua na kuthamini mchango wa wataalamu katika sekta mbalimbali ni nyenzo muhimu inayochochea maendeleo,pia huongeza ari ya utendaji kazi na kuleta matokeo chanya yenye manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Pia, amesema kuwa,kutambuliwa kwa juhudi na mchango wa kitaalamu si tu kunaleta motisha kwa wahusika, bali pia kunasaidia kuimarisha ubunifu, uwajibikaji na dhamira ya kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Amesema,utambuzi huo ni ishara ya kuthamini kazi kubwa inayofanywa na wataalamu wa teknolojia ya habari katika kukabiliana na changamoto zinazoibuka kutokana na matumizi ya mifumo ya kidijitali, hususan katika kipindi ambacho dunia inaendelea kushuhudia ongezeko la vitisho vya kimtandao.
“Utambuzi ni kichocheo cha kimkakati kinachobadilisha ari ya utendaji kazi kuwa matokeo yenye tija kwa taasisi, uchumi na wananchi. Kutambuliwa kwa mchango wa kitaalamu kunanipa nguvu zaidi ya kuendelea kushiriki katika juhudi za kulinda mazingira ya kidijitali na kuimarisha usalama wa taarifa nchini,”amesema Kileo.
Aidha, amesisitiza kuwa kujenga na kuendeleza utamaduni wa kutambua mchango wa wataalamu na watendaji bora ni hatua muhimu katika kuhifadhi na kuendeleza vipaji vya hali ya juu vinavyohitajika katika sekta nyeti kama usalama wa mtandao.
Kwa mujibu wa Kileo, uwekezaji katika rasilimali watu pamoja na kuthamini mchango wao huchochea ubunifu na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu, jambo ambalo hatimaye huwanufaisha wananchi kupitia huduma salama, bora na zenye kuaminika.
Ameongeza kuwa,maendeleo ya teknolojia yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi na wataalamu wa teknolojia ili kuhakikisha mifumo ya kidijitali inalindwa dhidi ya uhalifu wa mtandao na vitisho vingine vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taarifa na uchumi wa kidijitali.
Kauli hiyo imekuja katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika utoaji wa huduma mbalimbali, huku umuhimu wa usalama wa mtandao ukiendelea kupewa kipaumbele kama sehemu ya kulinda maslahi ya taifa na watumiaji wa huduma za kidijitali.