NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema, itaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kuchukua hatua madhubuti za kuvunja mitandao ya wahalifu, kutaifisha mali zinazotokana na biashara hiyo na kuimarisha huduma za tiba na urekebishaji wa waathirika.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Tume ya Uchaguzi Maisara Wilaya ya Mjini, Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais amesema,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kudhibiti uhalifu wa dawa za kulevya, ikiwemo kuanzisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, hatua inayolenga kuimarisha uratibu wa vita dhidi ya biashara na matumizi ya dawa hizo.
Amesema Zanzibar, ikiwa sehemu ya jumuiya ya kimataifa, inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku hiyo kwa kutambua kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni changamoto kubwa inayoendelea kuhatarisha maendeleo ya jamii, hususan kwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.
“Tatizo la dawa za kulevya linaendelea kuyakabili mataifa mengi duniani. Vijana ndiyo wanaoathirika zaidi, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki katika mapambano haya ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho,”amesema.
Mhe. Hemed amesema,Serikali imejipanga kuvunja mitandao ya wahalifu wakubwa wa dawa za kulevya, kuwachukulia hatua za kisheria wahusika pamoja na kutaifisha mali zinazotokana na biashara hiyo haramu, bila kujali wahusika ni wa ndani au nje ya nchi.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za tiba, ushauri nasaha na marekebisho ya tabia kwa kujenga vituo maalumu vya kuwahudumia waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya ili kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida.
Hata hivyo, amebainisha kuwa bado kuna changamoto zinazokwamisha juhudi hizo, ikiwemo kubadilika kwa mbinu zinazotumiwa na wahalifu katika kuzalisha na kusambaza dawa za kulevya.
Amesema,wahalifu wameanza kutengeneza dawa mpya za kulevya zenye kemikali tofauti na zile za asili kama bangi, cocaine na heroin, huku baadhi ya dawa hizo zikifichwa kwenye bidhaa zinazotumiwa na watu kila siku kama pipi, chokoleti, biskuti na sigara za kielektroniki.
Pia ameeleza kuwa,matumizi ya teknolojia na mitandao ya kijamii yameongeza changamoto ya biashara hiyo haramu kutokana na wahalifu kutumia majukwaa ya kidijitali kuwafikia na kuwashawishi vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.
Kutokana na hali hiyo, Makamu wa Pili wa Rais ametoa wito kwa wazazi, walezi, viongozi wa dini, walimu na jamii kwa ujumla kuongeza juhudi katika malezi ya watoto na vijana kwa kuimarisha maadili, elimu na mawasiliano ndani ya familia.
Amesisitiza kuwa,familia ndiyo ngome ya kwanza ya kuwakinga watoto dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, akionya kuwa taifa linaweza kupoteza nguvu kazi muhimu ikiwa jamii haitachukua hatua za pamoja katika kukabiliana na tatizo hilo.
“Malezi bora yanaanza nyumbani. Wazazi na walezi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao, kuwafundisha maadili mema na kuwapa mwongozo sahihi ili wasiingie katika makundi yanayohusika na matumizi ya dawa za kulevya,”amesema.
Aidha, ameagiza taasisi na vyombo vyote vinavyohusika na mapambano dhidi ya dawa za kulevya kuendelea kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa sheria, kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma na kutumia mbinu za kisasa kukabiliana na mitandao ya biashara hiyo haramu.
Amesema,mafanikio ya vita dhidi ya dawa za kulevya yanategemea ushirikiano wa Serikali, taasisi mbalimbali na wananchi, huku akisisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kushiriki katika kulinda afya, usalama na ustawi wa jamii.
