NA DIRAMAKINI
MSHAURI wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto,Mheshimiwa Ummy Ally Mwalimu amezitaka nchi za Afrika kuimarisha uongozi wa kisiasa,kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya na kuharakisha utekelezaji wa afua zilizothibitishwa kisayansi ili kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vya wajawazito, watoto wachanga,watoto na vijana.
Mheshimiwa Ummy ametoa wito huo Julai 8, 2026 aliposhiriki Warsha ya Uthibitishaji wa Sera kuhusu Afya ya Uzazi, Mama,Mtoto Mchanga,Mtoto na Vijana (SRMNCAH) kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, iliyoandaliwa na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) jijini Nairobi, Kenya.
Warsha hiyo imewakutanisha wawakilishi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, watunga sera, Tume ya Umoja wa Afrika, viongozi wa kikanda wakiwemo Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki,Kati na Kusini (ECSA Health Community).
Sambamba na washirika wa maendeleo ikiwemo UNICEF,UNFPA na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa lengo la kuthibitisha sera zitakazosaidia kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama, mtoto mchanga,mtoto na vijana barani Afrika.
Akizungumza katika warsha hiyo,Mheshimiwa Ummy amesema Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, imeendelea kuhimiza mataifa ya Afrika kuweka afya ya wanawake, watoto na vijana kuwa miongoni mwa vipaumbele vya maendeleo.
Amesema,dhamira ya Rais Samia ni kuendelea kuhamasisha uongozi wa kisiasa, kuimarisha uwajibikaji, kukuza mifumo endelevu ya upatikanaji wa rasilimali fedha na kuharakisha utekelezaji wa afua zinazotegemea ushahidi wa kisayansi ili kuboresha afya na ustawi wa wanawake, watoto wachanga,watoto na vijana katika bara zima la Afrika.
Mheshimiwa Ummy ameeleza kuwa,licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya, bado bara la Afrika linakabiliwa na changamoto kubwa za vifo vya akina mama wakati wa ujauzito na kujifungua, pamoja na vifo vya watoto wachanga na watoto wadogo vinavyoweza kuzuilika.
Amesema,watoto wengi bado hufariki ndani ya mwezi wao wa kwanza baada ya kuzaliwa, huku mamilioni ya watoto wengine wakiendelea kukosa chanjo muhimu zinazowalinda dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.
"Vifo vya wajawazito na watoto wadogo vinaweza kuzuilika kwa kiwango kikubwa. Changamoto tuliyonayo si ukosefu wa suluhisho, bali ni kuhakikisha afua zilizothibitishwa kisayansi zinatekelezwa kwa kiwango kikubwa, zinapata ufadhili endelevu na zinazingatia uwajibikaji ili kutoa matokeo yaliyokusudiwa,"amesema.
Amesisitiza kuwa,nchi za Afrika zina wajibu wa kushirikiana katika kuimarisha mifumo ya afya, kuongeza uwekezaji katika huduma za afya ya uzazi na mtoto pamoja na kuhakikisha sera zinazopitishwa zinatekelezwa kwa ufanisi ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Aidha, amesema afya bora ya wanawake, watoto na vijana ndiyo msingi wa kujenga rasilimali watu yenye uwezo wa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika bara la Afrika.
Alihitimisha kwa kusisitiza kuwa,wadau wote wanapaswa kushirikiana kuhakikisha kila mwanamke anapata huduma salama wakati wa ujauzito na kujifungua, kila mtoto anaanza maisha akiwa na afya njema na kila kijana anapata fursa ya kufikia uwezo wake kamili.
"Kwa pamoja tuna wajibu wa kuhakikisha hakuna mwanamke anayepoteza maisha kutokana na ujauzito au kujifungua, kila mtoto anapata mwanzo bora wa maisha, na kila kijana anapata fursa ya kufikia ndoto zake. Hii ndiyo njia ya kujenga Afrika yenye afya, ustawi na maendeleo endelevu,"amesema Mheshimiwa Ummy.









