NA DIRAMAKINI
BARAZA la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limewasimamisha Masheikh wa mikoa mitatu baada ya kubainika kwa kile kilichoelezwa kuwa ni mwenendo unaokiuka misingi ya kiuongozi ya baraza hilo.

Sheikh Walid Alhad Kawambwa.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha dharura cha Baraza la Ulamaa kilichofanyika leo Julai 14, 2026 na kuongozwa na Kaimu Mufti na Naibu Kadhi Mkuu wa Tanzania,Sheikh Ally Khamisi Ngeruko.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Hassan Said Chizenga, Masheikh waliosimamishwa ni Sheikh Walid Alhad Kawambwa, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam; Sheikh Issa Nassor Issa, Sheikh wa Mkoa wa Singida; na Sheikh Hassan Kiburwa, Sheikh wa Mkoa wa Kigoma.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa,uamuzi huo umeanza kutekelezwa rasmi kuanzia leo Julai 14, 2026, huku ikieleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa kuzingatia taratibu na misingi ya uongozi wa BAKWATA.
Wakati huo huo, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dkt.Abubakar Zubeir Mbwana amefanya uteuzi wa viongozi wa muda watakaosimamia ofisi hizo hadi pale maamuzi mengine yatakapofikiwa na mamlaka husika.
Kwa mujibu wa uteuzi huo, Sheikh Abasi Ramadhani Abasi ameteuliwa kuwa Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Issa Ramadhani Simba kuwa Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida, huku Sheikh Uwesu Mohamed Kiumbe akiteuliwa kuwa Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Kigoma.
BAKWATA imeeleza kuwa,viongozi hao wa muda watasimamia shughuli za kiutawala na kidini katika mikoa husika ili kuhakikisha huduma na majukumu ya taasisi hiyo yanaendelea kutolewa bila kuathiriwa na mabadiliko ya kiuongozi yaliyofanyika.
Aidha, Baraza hilo limeielekeza Ofisi ya Katibu Mkuu wa BAKWATA kusimamia mchakato wa makabidhiano ya ofisi hizo kwa haraka ili viongozi walioteuliwa waanze kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa taratibu za taasisi.
Hata hivyo, taarifa ya Baraza la Ulamaa haikufafanua kwa kina sababu mahususi zilizosababisha kusimamishwa kwa Masheikh hao, zaidi ya kueleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na mwenendo unaodaiwa kukiuka misingi ya kiuongozi ya Baraza.
Hatua hiyo inaashiria dhamira ya BAKWATA ya kuendelea kusimamia misingi ya uongozi, uwajibikaji na nidhamu ndani ya taasisi hiyo, huku ikisisitiza umuhimu wa viongozi wake kuzingatia taratibu, kanuni na maadili yanayoongoza utendaji wa Baraza.