BoT yanunua tani 28 za dhahabu ndani ya miezi 18, Gavana Tutuba aeleza mafanikio ya mpango huo

BANJUL-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba amesema kwamba katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, Benki Kuu ya Tanzania imenunua na kuhifadhi takriban tani 28 za dhahabu, zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.68 (thamani ya dhahabu iliyopo kwa bei ya jana), sawa na shilingi trilioni 9.76, ikiwa ni Mkakati wa Serikali wa kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, thamani ya shilingi, uthabiti wa sekta ya fedha na ukuaji wa uchumi.
Bw. Tutuba ameyasema hayo aliposhiriki mjadala kuhusu Mikakati ya Ununuzi wa Dhahabu ya Benki Kuu ikiwa ni sehemu ya mijadala ya Mkutano wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), African Caucus 2026, unaozihusisha nchi 54 za Afrika, unaofanyika Banjul nchini Gambia.

Amesema kuwa,mpango huo wa kununua dhahabu si tu kwamba umeiwezesha nchi kuhifadhi dhahabu kama mbadala wa kutunza fedha za kigeni, lakini pia umeongeza urasimishaji kwenye sekta ya madini na ujumuishi wa kifedha kwa wauza madini hayo, wakiwemo wachimbaji wadogo, ambapo Benki Kuu imewezesha makundi hayo kufungua zaidi ya akaunti 4,000 katika taasisi mbalimbali za fedha hususan benki.
Gavana Tutuba ameeleza kuwa,kutokana na bei nzuri ya soko ambayo Benki Kuu inatoa kwa wafanyabiashara wa madini, kumekuwa na mwitikio chanya wa wafanyabiashara na wachimbaji kuiuzia dhahabu Benki Kuu ya Tanzania.

“Tunawalipa wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu kwa wakati, ndani ya saa 24 tangu kufanyika kwa mauzo, na tunawalipa kwa bei ya soko la dhahabu la London ya siku hiyo, hatua inayowavutia kuiuzia dhahabu Benki Kuu,"amesema Gavana Tutuba.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), na umewashirikisha pia Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria anaye hudumia pia shughuli za kibalozi katika nchi ya Gambia, Mhe. Balozi Selestine Kakele.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here