MTWARA-Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limeendelea kuhamasisha wananchi kuchukua hatua za kuhakikisha visima vinajengwa kwa kuzingatia viwango vya usalama, ikiwemo kuvifunika na kuvizungushia uzio, ili kulinda afya za wananchi na kuzuia ajali zinazoweza kusababisha vifo au majeraha.
Elimu hiyo imetolewa kwa wananchi wa Kijiji na Kata ya Sululu Wilaya ya Masasi na Polisi Kata wa Sululu, Sajenti wa Polisi Eneck William wakati wa ziara ya kutoa elimu ya usalama katika kaya mbalimbali za kijiji hicho.
Akizungumza na wananchi, Sajenti William amesema kuwa, visima visivyofunikwa au visivyojengewa uzio vinaweza kuwa chanzo cha ajali kwa watoto, wazee na watu wenye mahitaji maalum, pamoja na kusababisha uchafuzi wa maji unaoweza kuibua magonjwa ya mlipuko.
Amesisitiza kuwa, wananchi wanapaswa kuhakikisha visima vyote vinajengwa katika maeneo salama na vinatunzwa kwa kufuata taratibu za afya na usalama wa mazingira.
Aidha, amewatahadharisha wananchi kuacha kuchimba visima katika makutano ya barabara za mitaa, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara na kuongeza uwezekano wa kutokea kwa ajali.
Sajenti William amesema kuwa,usimamizi mzuri wa visima utasaidia kulinda maisha ya watu na mifugo, kuzuia upotevu wa nguvu kazi ya Taifa na kupunguza gharama zinazoweza kujitokeza kutokana na ajali au milipuko ya magonjwa yanayosababishwa na maji yasiyo salama.
Kwa upande wake, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limeeleza kuwa,kupitia mpango wa Polisi Kata linaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya usalama na afya ya jamii, ikiwa ni pamoja na matumizi salama ya visima.
Jeshi hilo limewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kutekeleza hatua za kujikinga na hatari zinazoweza kuepukika, likisisitiza kuwa visima vinapaswa kuwa chanzo cha huduma muhimu ya maji kwa jamii na si sababu ya majanga yanayoweza kuzuilika.
