NA DIRAMAKINI
KAMPUNI ya Ufaransa ya Canal+ imeanza kutekeleza mkakati mkubwa wa kuibadilisha MultiChoice, kampuni inayomiliki huduma ya televisheni ya DStv huku ikiripoti kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya wanachama wapya hadi kufikia kiwango cha juu zaidi kwa zaidi ya muongo mmoja.
Canal+, ambayo mwaka 2025 ilichukua udhibiti wa MultiChoice kupitia mkataba uliokuwa na thamani ya zaidi ya rand bilioni 50, imeanza kufanya mabadiliko kadhaa makubwa katika uendeshaji wa kampuni hiyo, ikiwa ni pamoja na kusitisha huduma ya Showmax na kuhamishia jijini Paris baadhi ya maamuzi kuhusu maudhui kwa soko la Afrika Kusini.
Katika matokeo yake ya nusu mwaka 2026, Canal+ imesema mkakati huo wa mageuzi umeanza kuonesha matokeo, huku upatikanaji wa wanachama wapya katika nchi ambazo MultiChoice inafanya biashara ukiongezeka kwa asilimia 40 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Kampuni hiyo imesema Juni 2026 ulikuwa mwezi wenye ongezeko kubwa zaidi la wanachama wapya nchini Afrika Kusini katika kipindi cha miaka 10.
Mtandao wa mauzo nao wapanuliwa
Canal+ pia imeongeza mtandao wa mauzo wa MultiChoice, ambapo idadi ya vituo vya mauzo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 15 tangu Machi 2026.
Hatua nyingine iliyochukuliwa ni kupunguza bei ya vifaa kwa wanachama wapya, jambo ambalo kampuni imesema linalenga kupunguza gharama ya kuanza kutumia huduma na kuvutia wateja wengi zaidi.
Kwa upande wa maudhui, Canal+ imesema imeendelea kuimarisha ofa zake kwa kupata haki za muda mrefu za kuonesha Ligi Kuu ya England (Premier League) nchini Afrika Kusini, pamoja na Kombe la Dunia la Rugby la Wanaume 2027 na la Wanawake 2029 katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kampuni hiyo pia imeeleza kuwa imeendesha kampeni mbalimbali za maudhui na masoko, ikiwemo kampeni ya Kombe la Dunia iliyomhusisha mwigizaji maarufu Idris Elba, pamoja na kuzindua chaneli ya Novelas+ nchini Afrika Kusini.
Uzalishaji wa maudhui ya Afrika Kusini
Katika hatua nyingine, uzalishaji umeanza kwa filamu kubwa ya kwanza ya Afrika Kusini iitwayo The Road Home, The Heist of Benin, huku pia kukiwa na maandalizi ya kutengeneza filamu inayotokana na riwaya maarufu Americanah ya mwandishi Chimamanda Ngozi Adichie.
Hatua hizo zinaashiria mkakati wa Canal+ wa kuendeleza maudhui yanayolenga hadhira ya Afrika pamoja na kuongeza mvuto wa huduma zake katika soko hilo.
Mapato na faida ya MultiChoice yapanda
Kwa upande wa fedha, MultiChoice Group imerekodi ongezeko kubwa katika faida yake ya uendeshaji iliyorekebishwa kabla ya gharama maalumu (Adjusted EBIT before exceptional items), ambayo imeongezeka kwa asilimia 160 hadi kufikia €143 milioni, sawa na takribani rand bilioni 2.7.
Canal+ imesema ongezeko hilo limetokana kwa kiasi kikubwa na manufaa ya kuunganisha shughuli za kampuni hizo (synergies) pamoja na athari ya kifedha ya €120 milioni, sawa na takribani rand bilioni 2.2, ikiwemo athari za kusitishwa kwa huduma ya Showmax.
Mkurugenzi Mtendaji wa Canal+, Maxime Saada amesema,msingi wa mkakati huo ni kuongeza idadi ya wanachama huku kupunguza gharama za kuanza kutumia huduma na kupanua mtandao wa mauzo.
“Barani Afrika, tumeongeza idadi ya wanachama wetu kwa asilimia 7, na kama sehemu ya mpango wa mageuzi ya MultiChoice, tumepunguza gharama za kuanza huduma kwa wanachama wapya na kupanua mtandao wetu wa mauzo,"amesema Saada.
Mapato ya Canal+ yaongezeka kwa asilimia 40
Kwa ujumla, mapato ya Canal+ Group yaliongezeka kwa asilimia 40 hadi kufikia €4.287 bilioni, sawa na takribani rand bilioni 81.76, ongezeko ambalo kwa kiasi kikubwa limehusishwa na kuanza kujumuisha mapato ya MultiChoice katika hesabu za Canal+.
Faida ya uendeshaji iliyorekebishwa kabla ya gharama maalumu (Adjusted EBIT before exceptional items) nayo iliongezeka kwa asilimia 68 hadi kufikia €433 milioni, sawa na takribani rand bilioni 8.26, ikiwa na kiwango cha faida cha asilimia 10.1.
Canal+ imeeleza kuwa ongezeko hilo limechangiwa zaidi na kuongezeka kwa ukubwa wa kundi baada ya kuunganisha MultiChoice katika shughuli zake.
Hata hivyo, licha ya ongezeko hilo la mapato na faida ya uendeshaji, mapato halisi yanayohusishwa na wamiliki wa hisa wa kampuni mama yalishuka kutoka €70 milioni hadi €29 milioni, huku mapato kwa kila hisa yakishuka kutoka €0.07 hadi €0.03.
Canal+ yaendelea kujiamini na malengo ya 2026
Canal+ imesema bado iko katika njia ya kufikia malengo yake ya mwaka 2026, ambayo ni kupata €250 milioni za Adjusted EBIT na €220 milioni za mtiririko huru wa fedha (free cash flow).
Saada amesema,matokeo ya nusu ya kwanza ya mwaka yanaonesha kuwa mkakati wa kampuni unaendelea kupata mafanikio, akibainisha kuwa ongezeko la mapato na faida ya uendeshaji limetokana kwa kiasi kikubwa na ukubwa mpya wa kampuni baada ya kuichukua MultiChoice.
| Results in euros | Unaudited H1 2026 | H1 2025 Restated | Change (%) |
| MultiChoice Group | |||
| Revenues | 1,184 | 1,220 | -2.9% |
| Adjusted EBIT (EBITa) before exceptional items | 143 | 107 | 34.4% |
| As a percentage of total consolidated revenues | 12.1% | 8.7% | |
| of which revenues elimination linked to MultiChoice Group | (24) | (29) |
Kwa mtazamo mpana, mabadiliko hayo yanaashiria enzi mpya kwa MultiChoice na DStv, huku Canal+ ikilenga kuunganisha nguvu za kampuni hizo, kuongeza wanachama, kupanua mtandao wa mauzo, kuimarisha maudhui na kupunguza vikwazo vya gharama kwa wateja wapya.
Hatua ya kusitishwa kwa Showmax na kuimarishwa kwa DStv chini ya mkakati mpya wa Canal+ pia inaashiria mabadiliko makubwa katika ushindani wa huduma za televisheni na maudhui ya kidijitali katika soko la Afrika.(BT)
