Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kitaendelea kusaidia Serikali kufikia malengo ya Dira 2050-Mwanasheria Mkuu wa Serikali

ARUSHA-Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA), Mheshimiwa Hamza S. Johari amesema,chama hicho kitaendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya Taifa kwa kuhakikisha ushauri wa kisheria,utungaji wa sheria na usimamizi wa mikataba vinaendelea kulinda maslahi ya umma na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Johari ameyasema hayo leo Julai 13, 2026 wakati akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) uliofunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) jijini Arusha.

Mheshimiwa Johari amesema, TPBA imeendelea kukua na kuwa jukwaa muhimu la kukuza taaluma ya sheria kupitia kubadilishana uzoefu, kujengeana uwezo, kuimarisha maadili ya kazi na kuongeza ushirikiano miongoni mwa mawakili wa Serikali wanaofanya kazi katika taasisi mbalimbali za umma.

Amesisitiza kuwa,chama cha kitaaluma kinapaswa kuwa sehemu ya suluhisho katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali badala ya kuwa chanzo cha kuyumbisha utendaji wake.

"Chama bora cha kitaaluma ni kile kinachosaidia Serikali katika kufikia malengo yake na si kuitikisa au kuiyumbisha Serikali," amesema Mheshimiwa Johari.

Ameeleza kuwa,mkutano huo wa siku mbili unalenga kuwapa wanachama fursa ya kujadili maendeleo ya chama,masuala yanayohusu sekta ya sheria nchini pamoja na kufanya uchaguzi wa viongozi watakaoongoza TPBA katika kipindi kijacho.

Vilevile,Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema,moja ya mafanikio makubwa ya TPBA ni uzinduzi wa kitabu cha "Mama Samia Doctrine of Law (Falsafa ya Sheria ya Mama Samia)", kinachoeleza kwa kina namna mageuzi ya kisheria yaliyofanyika katika Serikali ya Awamu ya Sita yalivyochangia maendeleo ya kiuchumi,kijamii na kiutawala.

Amesema,kitabu hicho kinafafanua jinsi Serikali ilivyotumia sheria, sera, taasisi na mifumo ya utekelezaji kujenga mazingira bora ya maridhiano, uwekezaji, uwazi, utoaji wa huduma, haki na maendeleo ya wananchi.

Kwa mujibu wa Mhe.Johari, falsafa hiyo imeonekana katika sekta mbalimbali zikiwemo kodi na mapato, uwekezaji, nishati, ardhi, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), utalii, elimu, huduma za msaada wa kisheria, hifadhi ya jamii, utawala bora pamoja na ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).
Sheria ni Chombo cha Maendeleo

Akizungumzia nafasi ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Johari amesema,ofisi hiyo ina jukumu la kuishauri Serikali kuhusu sheria, utungaji na tafsiri ya sheria, usimamizi wa mikataba pamoja na kulinda maslahi ya umma.

Amebainisha kuwa,ushauri wa kisheria una thamani kubwa pale unapowezesha Serikali kufanya maamuzi yanayopunguza migogoro, kulinda rasilimali za Taifa, kuvutia uwekezaji na kuhakikisha wananchi wanapata haki na huduma bora kwa wakati.

"Ushauri wa sheria una thamani zaidi pale unaposaidia Serikali kufanya maamuzi yanayolinda maslahi ya Taifa, yanayoleta maendeleo,yanayopunguza migogoro, yanayovutia uwekezaji na yanayowezesha wananchi kupata haki kwa wakati,"amesema.

Pia,Mheshimiwa Johari amesema,utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji mfumo wa sheria unaoendana na malengo ya maendeleo ya nchi, akibainisha kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt.Samia ya kupitia na kuoanisha sheria mbalimbali ili ziendane na mahitaji ya dira hiyo.

Amesema,ofisi yake itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuboresha sheria, kuimarisha ushauri wa kisheria kwa Serikali, kusimamia mikataba na kuhakikisha sheria zinaendelea kuwa nyenzo ya maendeleo ya Taifa.
Aishukuru Serikali kwa kuboresha mazingira ya kazi

Katika hotuba yake, Mheshimiwa Johari amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi katika sekta ya sheria, hususan Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Amesema,maboresho yaliyofanywa na Serikali yameongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo na kuwezesha mawakili wa Serikali kutoa huduma bora zaidi kwa Serikali na wananchi.

Mkutano Mkuu wa TPBA wa mwaka 2026 unafanyika kwa siku mbili kuanzia Julai 13 hadi 14, 2026 ukiwa na kaulimbiu isemayo, "Haki, Wajibu na Utawala wa Sheria ni Msingi wa Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050."

Washiriki wa mkutano huo wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya taaluma ya sheria, matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za kisheria, uimarishaji wa uwezo wa mawakili wa Serikali na mchango wa sekta ya sheria katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here