NA GODFREY NNKO
MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Mheshimiwa Sixtus Mapunda amewataka wananchi kukataa matumizi na biashara ya dawa za kulevya kwa vitendo na kwa dhati, akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya tatizo hilo hayawezi kufanikiwa ikiwa jamii itapinga dawa hizo kwa maneno pekee.
Mheshimiwa Mapunda ametoa kauli hiyo leo Julai 23, 2026 katika Viwanja vya Mwembeyanga,Temeke jijini Dar es Salaam, wakati akifungua mwendelezo wa tamasha la kuifikia na kuihamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya lililoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Amesema, juhudi zinazofanywa na DCEA chini ya uongozi wa Kamishna Jenerali, Aretas Lyimo, katika kukabiliana na usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya nchini zinastahili kuungwa mkono na jamii nzima.
Mkuu huyo wa Wilaya amempongeza Kamishna Jenerali Lyimo kwa jitihada za kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya, akisema programu ya kuifikia na kuhamasisha jamii ni hatua muhimu katika kuongeza uelewa wa wananchi na kuwahusisha moja kwa moja katika kutokomeza tatizo hilo.
Kwa mujibu wa Mhe.Mapunda, jiografia ya Wilaya ya Temeke inafanya suala la matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya kuwa changamoto inayohitaji ushirikiano wa Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi.Amesema, elimu inayotolewa na DCEA itasaidia wananchi kutambua madhara ya dawa za kulevya mapema, kuzungumza na watoto kuhusu hatari zake, kukataa vishawishi vya matumizi na kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na biashara ya dawa hizo.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao na kuwajengea uelewa kuhusu madhara ya dawa za kulevya, akisema malezi na mazungumzo ya wazi katika familia ni miongoni mwa njia muhimu za kuzuia vijana kuingia katika matumizi ya dawa hizo.
Amesema,jamii inapaswa pia kuwa makini na vishawishi vinavyoweza kuwafanya vijana kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na tamaa ya maisha ya anasa yanayoonyeshwa kupitia mitandao ya kijamii bila kuelewa chanzo cha utajiri huo.
Mhe. Mapunda amesisitiza pia umuhimu wa kuendelea kuvunja mitandao ya usambazaji wa dawa za kulevya, akisema wahusika katika biashara hiyo wamekuwa wakisababisha madhara makubwa kwa wananchi, hususan vijana na watu wenye kipato cha chini.
“Ndugu zangu wa Temeke, tukatae dawa za kulevya moyoni, siyo mdomoni. Kwani mkiendelea kukataa mdomoni badala ya moyoni, hii vita inakuwa ngumu,” amesema.
Amesema,dawa za kulevya ni tishio kwa usalama wa Taifa kwa kuwa zinadhoofisha nguvu kazi, kuharibu maisha ya vijana, kuongeza uhalifu na kuathiri ustawi wa familia na jamii kwa ujumla.
“Dawa za kulevya huwa zinaangusha Taifa, zinadondosha nguvu kazi na kulipeleka Taifa kwenye usalama wa mashaka. Hivyo tubebe ajenda ya dawa za kulevya kama adui wa usalama wa Taifa na muuaji wa jamii,” amesema.
DCEA
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa DCEA, Kamishna Msaidizi wa Tiba na Huduma za Utengamao wa Mamlaka hiyo, Dkt. Cassian Nyandindi amesema,tatizo la dawa za kulevya linahitaji jitihada shirikishi kutoka kwa Serikali, taasisi, familia na jamii kwa ujumla.
Amesema,DCEA inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha Tanzania inafikia lengo la kuwa nchi isiyo na dawa za kulevya.
Dkt.Nyandindi amesema,tamasha hilo ni sehemu ya jitihada za kuwaleta wananchi pamoja, kuwaelimisha na kuwahamasisha kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Amesema,tatizo hilo haliwezi kumuacha mtu yeyote salama, kwa kuwa hata kama mtu halimgusi moja kwa moja, linaweza kuathiri ndugu, jamaa, marafiki au jamii inayomzunguka.
Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa wananchi kote nchini kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika, kuelimisha jamii na kukataa kwa vitendo matumizi na biashara ya dawa hizo.
Aidha,ujumbe uliotolewa katika tamasha hilo umeendelea kusisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya si jukumu la Serikali pekee, bali ni ajenda ya kitaifa inayohitaji ushirikiano wa kila mwananchi ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho.Katika tukio hilo, wananchi na waraibu wa dawa za kulevya wameshiriki katika matembezi maalum ya kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Matembezi hayo yalianzia eneo la Kwa Azizi Ally na kuelekea Viwanja vya Mwembeyanga.
Tamasha hilo linajumuisha shughuli mbalimbali ikiwemo michezo, burudani na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)






