NA DIRAMAKINI
MAKAMU wa Rais na Waziri Mkuu wa Falme za Kiarabu (UAE) na Mtawala wa Dubai, Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum ameendelea kutekeleza mpango mpya wa kijamii unaoitwa “Bread for All” (Mkate kwa Wote) unaolenga kuhakikisha hakuna mtu anayekosa chakula kutokana na ukosefu wa uwezo wa kifedha.
Mpango huo unatoa mkate mpya bure kwa saa 24 kila siku kupitia mashine za kisasa zinazofanya kazi kiotomatiki na zilizowekwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dubai, hatua inayodhihirisha dhamira ya serikali ya kuimarisha ustawi wa jamii na kupunguza changamoto ya njaa.
Tofauti na mifumo ya kawaida ya misaada, huduma hiyo haihitaji mtu kujaza fomu, kusubiri uthibitisho wala kupitia taratibu zozote za kiutawala.
Aidha, imeundwa kwa namna inayolinda heshima na faragha ya wanaonufaika, hivyo kuondoa unyanyapaa ambao mara nyingi huambatana na kupokea misaada ya kibinadamu.
Kwa mujibu wa waandaaji wa mpango huo, mashine hizo za kisasa huandaa na kutoa mkate mpya muda wote wa mchana na usiku bila malipo kwa watu wenye uhitaji, huku zikiendeshwa kwa mfumo endelevu unaochanganya matumizi ya teknolojia na huduma za kibinadamu.
Mbali na kutoa mkate, mashine hizo pia zimewekewa mfumo unaowaruhusu wananchi na wadau mbalimbali kutoa michango ya hiari kwa njia rahisi ili kusaidia kuendeleza huduma hiyo na kuwafikia watu wengi zaidi wanaohitaji msaada.
Mpango wa Bread for All unatekelezwa kupitia ushirikiano kati ya Mohammed Bin Rashid Al Maktoum Global Initiatives na Mohammed Bin Rashid Global Centre for Endowment Consultancy, taasisi zinazojihusisha na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na misaada ya kibinadamu ndani na nje ya Falme za Kiarabu.
Kwa sasa, jumla ya mashine tano zimewekwa katika maeneo tofauti ya Dubai, huku matarajio yakiwa ni kupanua huduma hiyo kadri mahitaji yanavyoongezeka na kupata uungwaji mkono kutoka kwa wafadhili na wadau mbalimbali.
Uzinduzi wa mpango huo unaakisi dira ya Dubai ya kutumia teknolojia katika kuboresha maisha ya wananchi, kujenga jamii jumuishi na kuimarisha utamaduni wa kusaidiana, huku ukisisitiza kuwa upatikanaji wa chakula ni hitaji la msingi ambalo linapaswa kufikiwa na kila mtu bila ubaguzi.

