GST yakamilisha maandalizi ya watumishi kwa utafiti wa madini nchini

DODOMA-Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imekamilisha maandalizi ya watumishi watakaotekeleza shughuli za utafiti wa madini katika maeneo mbalimbali nchini kwa mwaka wa fedha 2026/2027, kwa kuunda timu za wataalamu kutoka kada mbalimbali zitakazotekeleza kazi hizo muhimu.
Akizungumza wakati wa kikao cha watumishi wa taasisi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Prof. Abdulkarim Mruma, uliopo katika Ofisi za GST jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa GST, Mhandisi Ally Samaje, alisema taasisi ina matarajio makubwa kuwa timu hizo zitafanya kazi kwa weledi, bidii na uzalendo ili kuzalisha matokeo yatakayochangia ukuaji wa sekta ya madini na maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Mhandisi Samaje amesema, shughuli za utafiti zitagharamiwa na fedha zilizotengwa na Serikali kupitia mapato yanayotokana na sekta ya madini, jambo linaloweka wajibu mkubwa kwa wataalamu kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yenye tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa kila timu inapaswa kuandaa mpango kazi unaozingatia taarifa na takwimu zilizopo katika maeneo ilikopangiwa kufanya kazi, ili kuongeza ubora wa utafiti na kuhakikisha matokeo yanayopatikana yanakuwa sahihi na yanayoweza kutumika katika kupanga maendeleo ya sekta ya madini.

Aidha, aliwataka wataalamu watakaotekeleza shughuli za utafiti katika maeneo ya Quarter Degree Sheets (QDS) kutambua maeneo yenye shughuli za wachimbaji wadogo na kuyapa kipaumbele, akieleza kuwa kundi hilo lina mchango mkubwa katika uzalishaji wa madini na ukuaji wa sekta hiyo nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kijiolojia wa GST, Alex Rutagwelela, aliwataka wataalamu kujifunza kwa haraka, kushirikiana na kufanya kazi kwa weledi ili kuendelea kujenga imani ya Serikali na wadau katika utekelezaji wa shughuli za utafiti wa madini.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Maabara, Bw. Notka Banteze, alisema mwongozo wa awali ulipendekeza utekelezaji wa programu hiyo kwa kipindi cha miaka sita, hivyo ni muhimu kuhakikisha kazi zinazofanyika zinazaa matokeo yanayoonekana na yenye kushawishi ili programu hiyo ikamilike kwa mafanikio na ikiwezekana iongezwe muda wa utekelezaji.

Akitoa ufafanuzi kuhusu maandalizi ya maeneo ya utafiti, Meneja wa Kanzidata ya Jiosayansi, Bw. Alphonce Bushi, alisema baadhi ya maeneo yaliyopangwa kufanyiwa utafiti tayari yanaendelea na shughuli za uchimbaji, hivyo aliwataka wataalamu kuhakikisha wanatengeneza ramani za jiolojia zenye ubora na usahihi zitakazowezesha kupatikana kwa taarifa sahihi za kijiolojia na kuongeza uelewa wa rasilimali zilizopo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Utawala na Uendeshaji, Bi. Neema Mhagama, aliwakumbusha watumishi kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, nidhamu na uwajibikaji wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao katika maeneo mbalimbali ya kazi.
Timu zilizoundwa zinajumuisha wataalamu kutoka kada za jiolojia, mafundi wa maabara na utafiti (Technicians), wataalamu wa ramani (Cartographers), wahandisi pamoja na madereva, ambao kwa pamoja watashiriki katika utekelezaji wa shughuli za utafiti wa madini zinazolenga kuongeza uelewa wa jiolojia ya Tanzania, kubaini maeneo mapya yenye fursa za madini na kuendelea kuimarisha usimamizi na maendeleo endelevu ya sekta ya madini nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here