RC Babu apokea tuzo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuimarisha utawala wa sheria Kilimanjaro

KILIMANJARO-Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu amepokea tuzo maalum kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutambua mchango wa mkoa katika kuimarisha utawala wa sheria, utoaji wa haki na ushirikiano na taasisi za kisheria.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo ofisini kwake, Mhe. Babu ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutambua juhudi zinazofanywa na Mkoa wa Kilimanjaro, kwani tuzo hiyo ni heshima kwa wananchi wa mkoa huo na motisha ya kuendelea kusimamia misingi ya utawala bora na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.

Aidha, amesema Mkoa wa Kilimanjaro utaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi zote za kisheria ili kuimarisha utoaji wa huduma za haki, kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya sheria na kuendelea kujenga jamii inayozingatia misingi ya utawala wa sheria.

Awali, akikabidhi tuzo hiyo, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Tamari Mdeme, amesema tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua ushirikiano mkubwa unaotolewa na uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro katika kuimarisha utawala bora wa kisheria na kuboresha upatikanaji wa huduma za haki kwa wananchi.

Bi. Tamari ameongeza kuwa ushirikiano unaotolewa na Mkoa wa Kilimanjaro, hususan kupitia Kamati za Ushauri wa Kisheria, umeendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa unachochea uwajibikaji, unaimarisha utatuzi wa migogoro kwa njia ya sheria na kuweka msingi wa suluhisho la kudumu kwa kero za wananchi, hatua inayochangia kuimarisha utawala wa sheria katika Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here