DAR-Mhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa,Dkt. Alphonce Temba maarufu kama Fire Man amesema aliongozwa na kile alichokitaja kuwa ufunuo wa kiroho Mtakatifu kutangaza mapema kuwa Timu ya Taifa ya Hispania ingetwaa Kombe la Dunia la FIFA 2026, matokeo ambayo yamekuja baada ya Hispania kuibuka bingwa wa dunia kwa kuifunga Argentina katika mchezo wa fainali.
Akizungumza leo Julai 20,2026 Dkt.Temba amesema,msimamo wake ulitofautiana na wachambuzi wengi wa soka na wadau wa michezo ambao walikuwa wakizipa nafasi kubwa timu za Argentina na Ufaransa kutwaa ubingwa huo.
Amesema,uzoefu wake kuhusu kuombea viongozi na sekta ya michezo ulianza mwaka 2011 baada ya kualikwa Ikulu ya Zambia na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo,hayati Michael Sata.
Kwa mujibu wa Dkt.Temba, kabla ya hapo alikuwa ametoa kauli mwaka 2007 kwamba Michael Sata angekuwa Rais wa Zambia.
Amesema,baada ya ushindi wa Sata katika uchaguzi, alialikwa Ikulu kwa maombi maalumu na kuweka agano la kuiombea nchi hiyo.
Aidha,amesema wakati wa maombi hayo Zambia ilikuwa ikijiandaa kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), na baada ya taifa hilo kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, alianza kuamini kuwa Mungu amempa neema ya kuliombea eneo la michezo.
Dkt.Temba amesema,katika miaka iliyofuata amekuwa akitoa kauli kuhusu matokeo ya baadhi ya mechi na timu mbalimbali, ikiwemo klabu ya Simba, ingawa hakuzipa uzito mkubwa hadi wakati wa Kombe la Dunia 2026 ambapo alisema alisukumwa zaidi kufuatilia mashindano hayo kwa kile alichokiita mwongozo wa Roho Mtakatifu.
Ameeleza kuwa,kadiri mashindano yalivyoendelea, alihisi wajibu mkubwa wa kutangaza kile alichoamini ameonyeshwa kiroho kuhusu matokeo ya michuano hiyo.
Katika mazungumzo hayo, Dkt.Temba ametoa wito kwa Serikali kumpa nafasi ya kukutana mapema na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kabla ya mashindano yajayo, akisema anaamini maombi yanaweza kuwajengea ari na kuwasaidia kufanya vizuri katika michuano ya CHAN 2027, ambayo Tanzania itaiandaa kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.
Pia ametangaza mpango wa kuanzisha vituo vya michezo nchini vitakavyolenga kusaidia vijana kupitia malezi ya kiroho na kuwahamasisha kutumia vipaji vyao kwa maendeleo ya taifa.
Dkt.Temba amedai kuwa,bado soka limekumbwa na imani mbalimbali zinazohusishwa na ushirikina na kuchukuliana nyota, akisisitiza kuwa kwa mtazamo wake maombi yana nafasi muhimu katika kuimarisha maadili, kuwajengea wachezaji imani na kuwatia moyo.
Akirejea maandiko ya Biblia kutoka Injili ya Mathayo 2:2–7 amesema, simulizi ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo inaonesha jinsi mamajusi walivyofuatilia nyota, akitumia mfano huo kueleza umuhimu wa viongozi wa dini kutumia vipawa vyao kuwasaidia watu.
Amesisitiza kuwa,kuombea taifa, viongozi na sekta mbalimbali, ikiwemo michezo, si suala la kidini pekee bali ni huduma kwa jamii inayolenga kuchangia amani, maendeleo na ustawi wa taifa bila kujali tofauti za imani.
Kauli za Dkt.Temba zinakuja wakati Tanzania ikiendelea na maandalizi ya kushiriki na kuwa mwenyeji mwenza wa michuano mbalimbali ya kimataifa, huku wadau wa michezo wakiendelea kujadili mbinu mbalimbali za kuimarisha ushindani wa timu za taifa katika ngazi ya kimataifa.

