Ilala yatangaza msako mkali dhidi ya madanguro,vitendo vya udhalilishaji

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Wilaya ya Ilala,Mheshimiwa Edward Mpogolo ametangaza kuanza kwa msako dhidi ya madanguro na vitendo vya ukiukwaji wa maadili katika wilaya hiyo, akisisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mtu yeyote anayejihusisha na biashara haramu au vitendo vinavyowahusisha watoto katika unyanyasaji na udhalilishaji.
Mpogolo ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda maadili ya jamii, usalama wa watoto na mustakabali wa kizazi kijacho.

Amesema,Serikali imepokea taarifa za vitendo vinavyodaiwa kufanyika katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Ilala ikiwemo Kata ya Zingiziwa, ambapo mtu mmoja anadaiwa kuwatumia watoto wa kike katika vitendo vya udhalilishaji kwa kuwachezesha wakiwa watupu kwa malipo ya kati ya Shilingi 3,000 na 5,000.

Ameeleza kuwa,vitendo hivyo ni vya kikatili, vinakiuka maadili ya jamii na vinahatarisha usalama pamoja na mustakabali wa watoto wanaopaswa kulindwa na jamii.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, mtuhumiwa wa tukio hilo tayari amekamatwa na Jeshi la Polisi na uchunguzi unaendelea ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo na hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.

“Niwapongeze sana Jeshi la Polisi kwa umakini wao.Wamechukua hatua mapema kabla madhara hayajaongezeka. Ushahidi uliopo utawezesha sheria kuchukua mkondo wake,” amesema.

Mpogolo amewataka wananchi kutokimbilia kumtetea mtu yeyote anayekabiliwa na tuhuma za kuhusisha watoto katika vitendo vya unyanyasaji au ukiukwaji wa maadili, akisisitiza kuwa uchunguzi wa vyombo vya dola unapaswa kupewa nafasi ili haki itendeke.

Aidha, amewataka wenyeviti wa mitaa, viongozi wa maeneo na wananchi kwa ujumla kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama katika kutoa taarifa kuhusu uwepo wa madanguro na vitendo vingine vinavyohatarisha maadili, usalama na ustawi wa jamii.

Amesisitiza kuwa,hakuna nafasi ya biashara au shughuli zinazowadhalilisha binadamu, kuharibu maadili ya jamii au kuwaweka watoto katika mazingira ya hatari.

Kwa mujibu wa Mpogolo, umaskini hauwezi kuwa sababu au kisingizio cha kuwahusisha watoto na wanawake katika vitendo vya udhalilishaji, akisema jamii ina wajibu wa pamoja wa kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya aina zote za unyanyasaji na unyonyaji.

Ameonya kuwa jamii ikifumbia macho vitendo hivyo, itakuwa inachangia kwa namna moja au nyingine kuhatarisha mustakabali wa kizazi kijacho.

Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza kuwa, mapambano dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa maadili yanahitaji ushirikiano wa Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa mitaa, wazazi na wananchi wote ili kuhakikisha mazingira ya jamii yanakuwa salama na yenye kulinda utu wa kila mmoja, hususan watoto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here