IMF yaidhinisha Dola milioni 443.9 kwa Tanzania,yasifu ukuaji wa uchumi na mageuzi ya kiuchumi

NA DIRAMAKINI

BODI ya Utendaji ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) imekamilisha tathmini ya sita na ya saba ya Mpango wa Extended Credit Facility (ECF) pamoja na tathmini ya tatu na ya nne ya Mpango wa Resilience and Sustainability Facility (RSF), hatua iliyowezesha Tanzania kupokea fedha za haraka zenye thamani ya SDR milioni 326.49, sawa na takribani Dola za Marekani milioni 443.9.
Uamuzi huo unaashiria hitimisho la utekelezaji wa programu hizo mbili ambazo zimekuwa zikiisaidia Tanzania kuimarisha uthabiti wa uchumi, kuendeleza mageuzi ya sera za kiuchumi na kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya IMF, Tanzania imeendelea kuonesha mafanikio makubwa ya kiuchumi kwa kurekodi ukuaji imara wa uchumi na kudumisha utulivu wa viashiria vya uchumi mpana.

Shirika hilo limesema, Pato la Taifa (GDP) lilikua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025, huku likitarajiwa kufikia wastani wa asilimia 6.2 katika kipindi cha kati, likichochewa na ukuaji wa sekta za madini, kilimo na utalii.

Katika fedha zilizoidhinishwa, SDR milioni 113.37 (takribani Dola za Marekani milioni 154.1) zinatolewa kupitia mpango wa ECF, na kufanya jumla ya fedha ambazo Tanzania imepokea kupitia mpango huo kufikia takribani Dola za Marekani bilioni 1.063.

Aidha, SDR milioni 213.12 (takribani Dola za Marekani milioni 289.7) zinatolewa kupitia mpango wa RSF, na hivyo kufanya jumla ya fedha zilizopatikana kupitia mpango huo kufikia takribani Dola za Marekani milioni 636.5.

IMF imeeleza kuwa,mpango wa ECF wa miezi 40 uliidhinishwa mwezi Julai,2022 kwa lengo la kusaidia kufufua uchumi, kudumisha uthabiti wa uchumi na sekta ya fedha pamoja na kukuza maendeleo jumuishi na endelevu. Mpango huo uliongezewa muda kwa miezi sita mwezi Juni 2024 na baadaye miezi mitatu mwezi Mei 2026.

Kwa upande wa RSF, mpango huo ulioanza Juni 2024 unalenga kusaidia mageuzi yatakayopunguza hatari za mizania ya malipo na kuongeza uwezo wa uchumi wa Tanzania kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika tathmini yake, IMF imebainisha kuwa utekelezaji wa programu ya mageuzi ya kiuchumi umeendelea kuwa wa kuridhisha.

Vigezo vyote vikuu vya utendaji vilivyowekwa hadi Juni 2025 vilifikiwa, huku malengo mengi ya Septemba na Desemba 2025 yalitekelezwa.

Aidha, taasisi hiyo imeeleza kuwa,vigezo vyote vinavyoendelea kutekelezwa vilifikiwa, huku hatua nne za mageuzi ya kimuundo zikitekelezwa kwa wakati na nyingine tatu zikikamilishwa baada ya kuchelewa. Pia, hatua tano za mageuzi chini ya mpango wa RSF zilikamilishwa, ingawa hatua tatu zinazohusu sekta ya nishati hazikufikiwa.

Kwa mujibu wa IMF, pamoja na ukuaji mzuri wa uchumi na mfumuko wa bei kubaki katika kiwango cha asilimia 4.0 mwezi Juni 2026, athari za kupanda kwa bei za mafuta duniani zinaanza kujitokeza katika uchumi wa Tanzania.

Shirika hilo limeeleza kuwa,nakisi ya urari wa biashara na huduma inatarajiwa kubaki katika kiwango kinachodhibitika kutokana na ongezeko la mauzo ya dhahabu nje ya nchi ambalo linaendelea kupunguza athari za kuongezeka kwa gharama za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kutokana na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, IMF imeonya kuwa hatari zinazoukabili uchumi zimeongezeka, ikieleza kuwa endapo mgogoro wa Mashariki ya Kati utaendelea kwa muda mrefu, unaweza kudhoofisha kasi ya ukuaji wa uchumi na kuongeza shinikizo la mfumuko wa bei.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IMF na Mwenyekiti Kaimu wa Bodi ya Utendaji, Bo Li amesema,programu ya mageuzi inayotekelezwa na Tanzania imeisaidia nchi kudumisha uthabiti wa uchumi licha ya changamoto za ndani na nje ya nchi.

Amesema,mageuzi hayo yameimarisha mifumo ya sera za uchumi na taasisi zake, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuboresha usimamizi wa fedha za umma na kuharakisha mageuzi ya kiuchumi ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Bo Li pia ameeleza kuwa,Tanzania inapaswa kuendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi wa jamii ili kupunguza umaskini, kuongeza uwekezaji katika sekta za elimu na afya pamoja na kuhakikisha deni la taifa linaendelea kuwa himilivu.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuendelea kufuatilia mwenendo wa mfumuko wa bei na kuwa tayari kuchukua hatua za sera za fedha pale itakapohitajika, sambamba na kudumisha akiba ya fedha za kigeni na kuboresha usimamizi wa sekta ya fedha.

Kwa upande mwingine, IMF imeeleza kuwa, mageuzi yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara, kukuza sekta binafsi na kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yatakuwa muhimu katika kuongeza ajira, kuvutia uwekezaji na kuhakikisha uchumi wa Tanzania unakuwa shindani na wenye ustahimilivu kwa muda mrefu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here