iTrust Bond yaorodheshwa rasmi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE)

NA GODFREY NNKO

HATIFUNGANI ya iTrust Bond imeorodheshwa rasmi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) leo Julai 8,2026 hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za uwekezaji na kuimarisha maendeleo ya soko la mitaji nchini.
Uorodheshaji huo unaashiria hatua muhimu katika kupanua wigo wa bidhaa za kifedha zinazopatikana katika soko la mitaji la Tanzania, huku ukiwapa wawekezaji binafsi na taasisi fursa zaidi za kuwekeza katika hatifungani kupitia soko rasmi la hisa.

Kupitia uorodheshaji huo, wawekezaji sasa wataweza kununua na kuuza hatifungani hiyo katika soko la upili la DSE, jambo litakaloongeza ukwasi wa uwekezaji na kurahisisha upatikanaji wa mtaji kwa miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo.

Wadau wa sekta ya fedha wanaeleza kuwa, hatua hiyo inaendelea kuonesha kukua kwa soko la mitaji nchini na juhudi za kuendeleza ubunifu wa bidhaa za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wawekezaji wa makundi mbalimbali.

Aidha, kuorodheshwa kwa iTrust Bond kunatarajiwa kuongeza ushiriki wa wananchi katika uwekezaji kupitia soko la mitaji, sambamba na kuimarisha utamaduni wa uwekezaji wa muda mrefu nchini.

Vilevile,uorodheshaji huo uliofanyika jijini Dar es Salaam ni sehemu ya jitihada za kuendelea kukuza sekta ya fedha na kuongeza upatikanaji wa vyanzo mbadala vya mtaji kwa uchumi wa Tanzania.

Hafla hiyo imeongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama ambapo imekuwa hatifungani ya kwanza nchini kwa kuweka rekodi ya makusanyo ya Shilingi Bilioni 114.12 dhidi ya lengo la awali la Shilingi Bilioni 15 ikiwa ni zaidi ya asilimia 760.78 nchini.

Akizungumza katika hafla ya kuorodheshwa kwa hatifungani hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa iTrust Finance, Faiz Arab amesema,muundo wa wawekezaji uliojitokeza umeonesha imani kubwa ya Watanzania katika bidhaa za uwekezaji zinazotolewa kupitia soko la mitaji.

Amesema,takwimu zinaonesha kuwa asilimia 66.66 ya wawekezaji walioshiriki katika iTrust Bond ni wawekezaji mmoja mmoja (Retail Investors), huku asilimia 33.34 wakiwa kampuni na taasisi (Institutional Investors).

Kwa mujibu wa Arab, ushiriki wa wawekezaji wa ndani ulikuwa mkubwa zaidi, ambapo asilimia 98.82 ya waliowekeza ni Watanzania, wakati asilimia 1.18 pekee ni wawekezaji wa kigeni.

Ameeleza kuwa,ushiriki huo mkubwa wa wawekezaji wa ndani unaashiria kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu fursa za uwekezaji kupitia soko la mitaji na unaweka msingi imara wa kukuza utamaduni wa uwekezaji nchini.

Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama amesema, kuorodheshwa kwa iTrust Bond katika Soko la Hisa la Dar es Salaam kumeongeza thamani ya uwekezaji katika hatifungani za kampuni na taasisi kwa asilimia 5.46, na kufikisha thamani ya soko hilo hadi Shilingi trilioni 2.20, kutoka Shilingi trilioni 2.09 kabla ya kuorodheshwa kwa hatifungani hiyo.

Amesema,ongezeko hilo linaimarisha zaidi maendeleo ya soko la mitaji nchini kwa kuongeza ukwasi (liquidity), jambo linalowezesha wawekezaji kununua na kuuza dhamana zao kwa urahisi zaidi.

"Ushiriki mkubwa wa wawekezaji mmoja mmoja wa ndani ni hatua muhimu katika kuongeza ukwasi wa soko la mitaji na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika shughuli rasmi za uwekezaji," amesema.

Ameongeza kuwa,hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Huduma za Kifedha (National Financial Inclusion Framework) unaolenga kupanua upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha na kuongeza ushiriki wa wananchi katika bidhaa mbalimbali za kifedha, ikiwemo uwekezaji kupitia soko la mitaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here