iTrust Bond yaweka historia DSE,yakusanya Shilingi bilioni 114.12 na kuvunja rekodi ya uwekezaji Tanzania

NA GODFREY NNKO

SOKO la mitaji nchini limeandika historia mpya baada ya Hatifungani ya iTrust Finance Limited (iTrust Bond) kuorodheshwa rasmi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) leo Julai 8,2026 huku ikivunja rekodi ya mauzo kwa kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 114.12, sawa na mafanikio ya asilimia 760.78 dhidi ya lengo la awali la Shilingi bilioni 15.
Mafanikio hayo yameifanya iTrust Bond kuwa hatifungani iliyopata mwitikio mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya masoko ya mitaji nchini, ikivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na MAKAZI Bond ya kampuni ya First Housing Finance Limited.

Akizungumza katika hafla ya kuorodheshwa kwa hatifungani hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama amesema, mafanikio hayo yanaonesha kuimarika kwa imani ya wawekezaji katika soko la mitaji la Tanzania na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyojengwa na Serikali.

CPA Mkama amesema, iTrust Bond imeweka historia kwa namna tatu muhimu. Kwanza, ni hatifungani ya kwanza kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam iliyotolewa na kampuni yenye leseni ya udalali wa masoko ya mitaji na usimamizi wa mifuko ya uwekezaji kutoka CMSA.

Pili, amesema mauzo ya awamu ya kwanza pekee yamezidi thamani ya mpango mzima wa hatifungani wa Shilingi bilioni 100 uliokuwa umepangwa kutolewa kwa awamu nne katika kipindi cha miaka minne.

"Tatu, hatifungani hii imepata mafanikio ya asilimia 760.78 baada ya kukusanya Shilingi bilioni 114.12 dhidi ya lengo la Shilingi bilioni 15, hivyo kuwa hatifungani iliyovunja rekodi zote zilizowahi kuwekwa nchini,"amesema CPA Mkama.

Amesema,mafanikio hayo yamechangiwa na maboresho mbalimbali yaliyofanywa katika soko la mitaji, ikiwemo kuondolewa kwa kodi ya zuio (withholding tax) kwenye mapato ya hatifungani za kampuni na taasisi.

Vilevile kupunguza kiwango cha chini cha uwekezaji kutoka Shilingi milioni moja hadi Shilingi 500,000 pamoja na kuidhinishwa kwa ulipaji wa riba kila baada ya miezi mitatu badala ya miezi sita.

CPA Mkama amesema,pia matumizi ya teknolojia yamekuwa kichocheo kikubwa cha mafanikio hayo, ambapo takribani asilimia 89 ya maombi yote ya uwekezaji yalifanyika kupitia mifumo ya kidijitali, huku programu ya iTrust App pekee ikichangia zaidi ya asilimia 71 ya maombi yote.

Aidha, amesema kuorodheshwa kwa iTrust Bond kumeongeza thamani ya uwekezaji katika hatifungani za kampuni na taasisi kwa asilimia 5.46, na kufikisha thamani ya soko hilo hadi Shilingi trilioni 2.20 kutoka Shilingi trilioni 2.09.












Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa iTrust Finance, Faiz Arab amesema,mwitikio wa wawekezaji umeonesha kuongezeka kwa imani ya wananchi katika bidhaa za uwekezaji zinazotolewa kupitia soko la mitaji.

Amesema,kati ya wawekezaji wote walioshiriki katika iTrust Bond, asilimia 66.66 walikuwa wawekezaji mmoja mmoja (Retail Investors), huku asilimia 33.34 wakiwa kampuni na taasisi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Arab, asilimia 98.82 ya wawekezaji walikuwa Watanzania, wakati asilimia 1.18 walikuwa wawekezaji wa kigeni, hali inayodhihirisha kuongezeka kwa ushiriki wa wananchi katika uwekezaji kupitia sekta rasmi ya fedha.

Aidha, amesema takribani asilimia 58 ya maombi yote ya uwekezaji yenye thamani ya Shilingi bilioni 66 yaliwasilishwa kwa njia za kidijitali, huku iTrust App pekee ikichangia maombi yenye thamani ya Shilingi bilioni 54, sawa na asilimia 47 ya fedha zote zilizoombwa.

Kutokana na mwitikio huo mkubwa, CMSA iliidhinisha iTrust Finance kupokea kiasi chote kilichoombwa na wawekezaji, hatua iliyowezesha wawekezaji wote waliokidhi vigezo kupata asilimia 100 ya kiasi walichoomba kuwekeza.

Hatifungani hiyo ina muda wa miaka minne, inalipa riba ya asilimia 13 kwa mwaka inayolipwa kila baada ya miezi mitatu, huku kiwango cha chini cha uwekezaji kikiwa Shilingi 500,000.

Arab amesema fedha zilizopatikana kupitia hatifungani hiyo zitatumika kupanua shughuli za kampuni kwa kuendeleza majukwaa ya kidijitali, kuongeza huduma za kifedha na kuimarisha utoaji wa mikopo inayotolewa kwa dhamana ya mali za mitaji.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Ally Othman amesema mafanikio ya iTrust Bond yanaonesha kuwa,soko la mitaji la Tanzania limeendelea kuwa jukwaa la kuaminika katika upatikanaji wa mtaji wa muda mrefu.

Amesema,licha ya hatifungani hiyo kulenga kukusanya Shilingi bilioni 15, ilipokea maombi yaliyovuka Shilingi bilioni 114, jambo linalodhihirisha imani kubwa ya wawekezaji kwa iTrust Finance na masoko ya mitaji nchini.

Kwa upande wa CRDB Bank Plc, mwakilishi wa benki hiyo na Mshauri Mkuu wa Miamala, Alexander Ngusaru amesema,mafanikio hayo yanaonesha uwezo wa taasisi za fedha za Tanzania kusimamia na kutekeleza miamala mikubwa ya masoko ya mitaji kwa viwango vya kimataifa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya iTrust Finance, Aunali Fidahussein Rajabali amewashukuru CMSA, DSE, CRDB Bank, washauri wa kisheria, wahasibu, wawekezaji na wafanyakazi wa kampuni kwa mchango wao uliofanikisha kuandikwa kwa historia hiyo.

Amesema, iTrust itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha na mamlaka za udhibiti katika kubuni bidhaa mpya za uwekezaji zitakazopanua fursa kwa Watanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia maendeleo ya soko la mitaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here